Bara la Afrika linahitaji haraka chanjo za COVID-19
5 Juni 2021Mkuu wa mpango wa chanjo wa shirika la afya duniani WHO, kitengo cha Afrika, Richard Mihigo ameiambia DW kwamba kati ya dozi milioni 66 zilizopaswa kutolewa barani Afrika chini ya mpango wa ugavi wa chanjo "COVAX”, ni dozi milioni 19 tu zilizopelekwa kwenye bara hilo. Wakati wastani wa chanjo zinazotolewa duniani kote ni asilimia 11, nchi za Afrika hazijafikia hata wastani wa asilimia 2. Ni asilimia 0.6 tu ya watu waliopatiwa chanjo zote mbili barani Afrika hadi sasa.
Shirika la afya duniani WHO na Benki ya dunia zimetahadharisha juu ya hatari ya kusimama kabisa mpango wa utoaji chanjo katika nchi za Afrika. Hata hivyo wadau wamesema hata ikiwa chanjo zinapelekwa, utoaji wake unatatizika, kutokana na changamoto za miundombinu. Baadhi ya nchi hata bado hazijaanza kutoa chanjo wakati baadhi ndio zinaaza sasa.
Waliokuwa na matumaini, hapo awali juu ya kuboreshwa ugavi wa chanjo katika nchi za Afrika sasa wamefadhaishwa. Mpaka sasa chanjo za BioNTech-Pfizer na Sinovac zimepelekwa kwenye nchi fulani kwa njia ya mapatano ya pande mbili. Nchi nyingi za Afrika hazina fedha za kuziwezesha kufikia mikataba na kampuni zinazotengeneza dawa hizo.
Kulingana na utafiti uliofanywa na shirika la DW, Uganda imepata dozi 864,000 kwa kupitia mpango wa COVAX na takriban zote zimeshatumika. Idadi hiyo haitoshelezi hata asilimia 2 ya watu wanaohitaji. Nchi nyingine 10 za Afrika tayari zimeshamaliza migao yao.
Baada ya dozi za kwanza kuwasili barani Afrika mwanzoni mwa mwaka huu chini ya mpango wa Covax, zoezi lilisimama kabisa mnamo mwezi Machi. Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la afya duniani WHO, bara la Afrika litakuwa na upungufu wa dozi zipatazo milioni 190 hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Juni. Uhaba huo umesababishwa na uamuzi wa India wa kusimamisha usafirishaji wa chanjo nje ya nchi baada ya kukumbwa na mawimbi makubwa ya maambukizi ya virusi vya corona.
Tatizo si uhaba wa chanjo tu unaoathiri juhudi zakutoa chanjo dhidi ya COVID-19. Mkuu wa mpango wa chanjo wa shirika la afya duniani WHO, kitengo cha Afrika Richard Mihigo amesema uhafifu wa miundombinu pia unachangia katika kuathiri juhudi za kutoa chanjo barani Afrika. Shirika la Afya Ulimwenguni limehimiza nchi tajiri kutoa misaada ya chanjo zao za ziada kupitia kwenye mpango wa ugavi wa COVAX.
Chanzo: https://p.dw.com/p/3uQsQ