1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barack Obama, Hilary Clinton na ushindani wa mwisho

Nijimbere, Gregoire3 Juni 2008

Nchini Marekani Hilary Clinton na Barack Obama, wanachuana leo katika hatua ya mwisho kabla ya uamuzi wa wajumbe wa chama mwezi Agosti mwaka huu juu ya muakilishi wa chama kwenye uchaguzi wa urais hapo Novemba mwaka huu.

Barack ObamaPicha: AP

Raia katika majimbo mawili ya Montana na Dakota ya kusini watakuwa ndiwo wa mwisho kumchagua atakayeshindana na muakilishi wa chama cha Republikan John Mc Cain kwenye uchaguzi wa urais ifikapo tarehe 4 Novemba mwaka huu. Majimbo hayo mawili yatawatuma wajumbe wake 31 kwenye mkutano mkuu wa wajumbe wote wa chama cha demokrate mwishoni mwa mwezi Agosti mjini Denver ambao ndiwo utaamuwa ni nani kati ya Barack Obama na Hilary Clinton akiwakilishe chama kwenye uchaguzi wa urais.


Licha ya kwamba Barack Obama bado anahitaji wajumbe kiasi ya 40 kutimiza idadi ya wajumbe 2118 inayotakiwa kuweza kuchaguliwa, anayo matumaini makubwa kuwapata wajumbe wa ngazi ya juu ambao ni jumla 200. Katika mkutano na waandishi wa habari hapo jana katika jimbo la Michigan, Barack Obama amesema na hapa ninamnukuu " kuna wajumbe kadhaa wa ngazi ya juu ambao wanasubiri matokeo ya uchaguzi katika majimbo hayo ya mwisho ili kuchukuwa msimamo na ninaamini hawatokawia kufanya hivyo", mwisho wa kumnukuu.


Kwa upande wake Hilary Clinton ambae licha ya kuwa nyuma kulingana na idadi ya wajumbe, amesema kwa vyote vile matokeo yatakavyokuwa katika majimbo hayo mawili ya Montana na Dakota ya kusini, ataendelea na kampeni yake kuwashawishi wajumbe wa ngazi ya juu wamchaguwe yeye.

Mmoja wa waungwaji mkono wakubwa wa Hilary Clinton aliye pia gavana wa jimbo la Pennsylvania Ed Rendell amesema " Mimi kusema kweli siamini kuwa Hilary Clinton atafanikiwa. Bila shaka seneta Barack Obama atakuwa amekwishapata wajumbe wanaohitajika hadi kufikia mwishoni mwa wiki hii. Ninafikiri Seneta Clinton atafanya kinachostahili kufanywa na kuchukuwa hatua kukiunganisha chama. Nasi sote tutamfuata", amemalizia kusema gavana Rendell.


Barack Obama alikuwa amepanga kusherehekea ushindi wake mara tu baada ya kumalizika uchaguzi huo wa Montana na Dakota na kuanzisha mara mmoja kampeni dhidi ya John Mc Cain wa chama cha Republikan. Waandamizi wa Barack Obama wamependelea wajumbe wa ngazi ya juu ambao hadi sasa hawajatangaza msimamo wao wafanye hivyo sasa hivi ili yote yajulikane kwa pamoja leo jioni ambapo kulingana na majira ya huko Marekani wanakopiga kura, itakuwa sawa na saa 9 alfasiri ya hapa Ujerumani. Lakini taarifa zinasema kundi la maseneta 17 kutoka chama cha demokrate wamekutana jana kulijadili swala hilo. Kuna uwezekano mkubwa wakasubiri matokeo ya majimbo hayo mawili ya mwisho ya Montana na Dakota ya kusini kumpa pia Hilary Clinton muda wa kukiri kushindwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW