Barani la Ulaya mwenyeji wa fainali za kombe la dunia 2018
1 Desemba 2010Kwa mara ya kwanza katika historia yake shirikisho la kandanda duniani, FIFA, litafanya uchaguzi wa nchi mbili zitakazokuwa wenyeji wa mashindano ya shirikisho hilo. Kamati tendaji itachagua leo Desemba 2 mjini Zurich nchi wenyeji wa mashindano ya soka kwa ajili ya fainali za kombe la dunia kwa mwaka 2018 pamoja na fainali za kombe hilo miaka minne baadaye. Rais wa FIFA, Joseph Blatter, anataka kuzipa nchi hizo zitakazochaguliwa nafasi ya muda mrefu wa kujitayarisha na ana matumaini kuwa hatua hiyo itasaidia kupata wadhamini wengi kupitia matangazo na televisheni .
Nchi zinazowania kuwa wenyeji wa mashindano hayo kwa ajili ya fainali za mwaka 2018 ni Uingereza, Urusi, Hispania na Ureno na Ubelgiji na Uholanzi. Kwa ajili ya fainali za mwaka 2022 wanaowania ni pamoja na Marekani, Australia, Katar, Korea ya kusini na Japan. Muda wa kuomba kuwa wenyeji kumekuwa na mivutano miongoni mwa wagombea. Uchaguzi huo ambao kura ni siri nao pia umegubikwa na shutuma kadha za rushwa dhidi ya wajumbe wa kamati hiyo tendaji, Amos Amadu kutoka Nigeria na Reynald Tenamrii kutoka Tahiti. Wajumbe hao wawili wamesimamishwa uwanachama kutokana na tuhuma hizo. Kamati hiyo tendaji , ya kile kinachojulikana kama serikali ya dunia inayoongoza soka, ina wajumbe 12, ambapo ni Franz Beckenbauer atakuwa mwanachama wake hadi 2011.
Katika uchaguzi huo ni wajumbe 22 tu ambao wanashiriki. Hali tayari ni wazi kuwa fainali za kombe la dunia kwa mwaka 2018 zitafanyika baada ya miaka 12 katika bara la Ulaya tangu yalipofanyika nchini Ujerumani. Marekani iliondoa ombi lake la kuwania kuwa mwenyeji wa kinyang'anyiro mapema mwezi wa Oktoba. Zikabakia nchi kutoka katika bara la Ulaya pekee. Nchi zinazoonekana kuwa mbele kuweza kupata kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ni pamoja na Uingereza na Urusi. Uingereza iliwahi kuwa mwenyeji wa fainali hizo katika mwaka 1966, na mwaka 1996 iliwahi kuwa mwenyeji wa mashindano ya fainali za kombe la mataifa ya Ulaya. Urusi haijawahi kuwa mwenyeji wa mashindano yoyote makubwa , na inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Olympiki ya majira ya baridi mwaka 2014. Katika mwaka 2012 nchini Uingereza kutakuwa na mashindano ya majira ya joto ya michezo ya Olympiki.
Uingereza inataraji kama inavyojulikana kuwa ni mama wa kandanda, kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa mara ya pili, baada ya ushindi wake wa fainali hizo mwaka 1966. Katika fainali iliishinda Ujerumani kwa mabao 4-2 baada ya dakika za nyongeza. Haitasahaulika lile goli linalojulikana nchini Ujerumani kama goli la Wembley, goli ambalo lilibishaniwa, lililofungwa na Geoff Hurst . Timu ya taifa ya Uingereza tangu wakati huo haijawahi kulinyakua tena kombe hilo, lakini ushiriki wa nchi hiyo katika mashindano haya haujasitishwa.
Urusi inajiona kuwa ni nchi ambayo inaweza kuwa mshindani mkubwa wa Uingereza katika kinyang'anyiro hicho cha kuwania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo. Tunataka kuonyesha hali mpya ya Urusi , anasema waziri wa michezo wa Urusi , Vitali Mutko. Pia tunataka kujaribu kujenga daraja baina ya kile watu wanachokifahamu kuhusu Urusi na hali halisi iliyopo. Hii ni nchi ambayo ina sura nyingi. Mfano wetu tunaupata kutoka Ujerumani, amesisitiza Mutko, kwamba jinsi Ujerumani ilivyochukulia kwa urahisi kupata ushindi wao ndivyo ilivyokuwa pia katika kuendesha mashindano hayo ya fainali za mwaka 2006. Pamoja na Urusi na Uingereza kuna nchi kama Ubelgiji na Uholanzi ambazo zina uzoefu wa kuwa wenyeji wa mashindano kama hayo.
Mwandishi : Boettcher, Arnulf / Sekione Kitojo/
Mhariri: Othman Miraji.