Baraza jipya la mawaziri latangazwa Libya
4 Oktoba 2011Mahmoud Jibril, ambaye ni mtaalamu wa mipango na mikakati aliyesomea Chuo Kikuu cha Pittsburgh, nchini Marekani, anabakia na nafasi yake ya uwaziri mkuu na anachukuwa pia nafasi ya uwaziri wa mambo ya nje, jambo linalomaamisha kuwa, naibu wake na aliyekuwa akishikilia wadhifa huo, Ali al-Issawi ametupwa nje.
Mwanauchumi aliyesomea Marekani pia, Ali al-Tarhouni, anaendelea na wadhifa wake wa uwaziri wa mafuta hadi hapo Shirika la Mafuta la Taifa litakapokuwa tayari kuchukuwa nafasi hii.
Mwansheria aliyewahi kujeruhiwa katika vita vya kumuondoa Gaddafi, Abdil-Rahman Al-Keissah, ameteuliwa kuwa waziri wa maafa na Hamza Abu Fas anachukuwa nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Sheikh Salim al-Sheikh kama waziri wa masuala ya dini.
Viongozi hawa wapya wamesema kuwa wataendelea kubakia kwenye nyadhifa zao hadi hapo nchi ikombolewe na iwe na utulivu kamili, ambalo serikali mpya ya mpito itaundwa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
"Tumechukuwa ahadi kwa Walibya kwamba hatutokuwamo kwenye serikali ijayo kwa namna yoyote ile." Mustafa Abdul-Jalil amewaambia waandishi wa habari mjini Benghazi.
Lakini hasa ni Mahmoud Jibril, ambaye wengi wa wapiganaji waliomuondoa Gaddafi madarakani wasiyemtaka awe sehemu ya serikali mpya. Wapiganaji hao wamekiambia kituo cha televisheni cha Al-Jazeera, kwamba wanamshuku Jibril kwa kupandikiza dhana ya kuwepo kwa Waislamu wenye siasa kali, ili apate huruma za mataifa ya magharibi, na kujiimarisha kwenye madaraka. Ismail Al- Sallabi, mmoja wa makamanda walioongoza vita dhidi ya Gaddafi na mpinzani mkubwa wa Jibril, mmefurahishwa na taarifa kwamba Jibril anakusudia kuondoka madarakani.
"Hii ni habari njema kwetu. Amewatenga wengi na amefanya makosa mengi. Alianzisha kampeni ya dhidi ya Waislamu wenye msimamo mkali. Sipendi jina hili. Sisi si Waislamu wenye siasa kali. Sisi ni wazalendo, wanamapinduzi wa kweli. Lakini Jibril alitumia dhana hii kutengeneza mgawanyiko kwenye nchi. Hiyo ndiyo sababu tunampinga." Amesema Al-Sallabi.
Wakati huo huo, taarifa kutoka Sirte, zinasema kwamba wapiganaji wa Baraza la Mpito wameshambulia ngome za Gaddafi kwenye mji huo, usiku wa kuamkia leo, na kufanikiwa kuingia hadi kwenye mji wa Qasr Abu Hadi. Mji huu wenye wakaazi 4,890 na ulio umbali wa kilomita 20 kusini mwa Sirte, ndipo hasa panaripotiwa kuzaliwa Gaddafi kwenye hema la wachungaji mwaka 1942. Kwa mujibu wa taarifa ni kuwa wapiganaji wameukuta mji huo ukiwa takribani umehamwa kabisa.
Wakaazi wachache waliokutikana kwenye mji wamewaambia waandishi wa habari kwamba wamejikuta katikati ya mapigano kati ya wafuasi wa Gaddafi na vikosi vya Baraza la Mpito.
Kwa wapiganaji wa Baraza la Mpito kuweza kuuchukuwa mji huu, kunaonekana kama ni ushindi mkubwa kwao. Hata hivyo, mjini Tripoli kwenyewe, Mkuu Mpya wa Baraza la Kijeshi, Abdel-Hakim Belhaj, ameamuru kutokuwepo kwa watu wenye silaha mitaani, akisema kwamba huko kunatishia amani ya wakaazi wa mji huo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFP/Reuters
Mhariri: Othman Miraji