Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lapinga mapinduzi ya Myanmar
18 Juni 2021Kwa mujibu wa taarifa za kidiplomasia,Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika mswada wa azimio hilo pia linalaani mauaji yanayofanywa na wanajeshi wa Myanmar. Umoja wa Mataifa pia unataka kuachiwa mara moja na bila ya masharti yoyote kwa kiongozi wa serikali ya kiraia Aung San Suu Kyi pamoja na vongozi wengine walioondolewa madarakani kwa nguvu na wengine wote waliotiwa ndani, kufunguliwa mashtaka au kukamatwa.
Waliopendekeza azimio hilo wanatumai kuwa litapitishwa kwa kura nyingi na hivyo kuwasilisha ujumbe wa nguvu kwa watawala wa kijeshi nchini Myanamar kwamba jumuiya ya kimataifa inapinga hatua iliyochukuliwa na wanajeshi ya kutwaa mamlaka mnamo tarehe mosi mwezi Februari. Mswada wa azimio hilo umetokana na mazungumzo ya jopo maalumu linalojumuisha nchi za Umoja wa Ulaya, nchi kadhaa za magharibi na za ukanda wa kusini mashariki mwa Asia.
Ikiwa mswada wa azimio hilo utapitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hiyo itakuwa hatua nyingine ya nadra ambapo baraza hilo la uwakilishi wa juu kabisa limejitokeza kupinga mapinduzi ya kijeshi na kutoa wito wa kuwekwa vikwazo.
Balozi wa Canada kwenye Umoja wa Mataifa, Bob Rae amesema kila mmoja amefanya kazi kwa bidii ili kufikia makubaliano ya wengi. Balozi Rae amesema mswada huo ni tamko kali la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la kupinga kinachoendelea nchini Myanmar na linaonyesha msimamo thabiti wa baraza hilo wa kutaka kuanzishwa mchakato wa kurejesha demokrasia, haki za kiraia na kiuchumi kwa wote ikiwa pamoja na watu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar.
Upinzani dhidi ya utawala wa kijeshi
Nchini Myanmar upinzani dhidi ya utawala wa kijeshi umeendelea kwa maandamano makubwa ya amani kote nchini. Hata hivyo baada ya wanajeshi kuanza kutumia nguvu kwa lengo la kuyazima maandamano hayo, raia pia walianza uasi wa kutumia nguvu mijini na mashambani.
Wiki iliyopita kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia haki za binadamu kilinukuu taarifa za kuaminika zinazothibitisha kwamba watu wapatao 860 wameuliwa na wanajeshi tangu mwezi Februari, wengi wao wakati wa maandamano na kwamba watu wengine zaidi ya 4800, miongoni mwao waandishi wa habari, wanaharakati na wapinzani wa utawala wa kijeshi wametiwa ndani kiholela.
Kwa muda wa miongo mitano Myanmar imekuwa inaongozwa chini ya tawala za kijeshi zilizosababisha kutengwa kwa nchi hiyo na jumuiya ya kimataifa. Hata hivyo baada ya wanajeshai kulegeza hatamu zao, kiongozi wa upinzani Suu Kyi aliruhusiwa kushiriki katika uchaguzi wa mwaka 2015 ambapo alishinda.
Jumuiya ya kimataifa iliitikia kwa kuondoa vikwazo kadhaa na kuanza kuwekeza vitega uchumi nchini Myanmar. Wanajeshi hawakufurahishwa na ushindi wa mwanasiasa huyo. Wanadai kwamba udanganyifu ulifanyika na ndipo waliamua kuuangusha uatwala wa kiraia wa San Suu Kyi kabla ya kikao cha bunge.
Katika mswada wake wa azimio, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linawataka watawala wa kijeshi nchini Myanmar waheshimu uamuzi wa wananchi katika uchaguzi wa mwaka 2015. Hata hivyo maazimzio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hayana meno ya kisheria.
Chanzo:/AP