1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNGA: Nini matarajio kutoka kwa viongozi wa dunia mwaka huu?

18 Septemba 2023

Viongozi mbalimbali wa dunia wameanza kuwasili mjini New York, Marekani, kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, UNGA, ambao unatazamiwa kugubikwa na vita nchini Ukraine pamoja na mzozo wa tabianchi.

Baraza la Umoja wa Mataifa | Hotuba ya Volodymyr Zelenskiy.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akihutubia kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, katika makao makuu ya UN mjini New York, Marekani, Septemba 21, 2022.Picha: Jason DeCrow/AP/picture alliance

Mgogoro wa tabianchi na vita nchini Ukraine vinatarajiwa kujitokeza pakubwa katika Umoja wa Mataifa wiki hii, huku zaidi ya viongozi 140 na wawakilishi wa nchi kutoka sehemu mbalimbali za dunia wakiwasili mjini New York kuhutubia kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Mkutano huo wa ngazi ya juu ambao unaanza rasmi hapo kesho Jumanne kufuatia wiki mbili za mikutano, ndiyo tukio linalofuatiliwa zaidi duniani katika kalenda ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa.

Unatoa fursa kwa viongozi wa dunia na wakuu wa nchi kuainisha vipaumbele vyao kwa mwaka unaokuja, kuhimiza ushirikiano juu ya masuala nyeti na kutoa wito kwa mahasimu wao.

"Ni wakati wa aina yake kila mwaka kwa viongozi kutoka kila pembe ya dunia sio tu kutathmini hali ya dunia bali kuchukua hatua kwa manufaa ya wote," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliwaambia waandishi wa habari wiki iliyopita. "Na hatua ndio ulimwengu unahitaji sasa."

Soma pia: Mkutano wa UN kujadili tena malengo ya maendeleo endelevu

Mjadala Mkuu wa mwaka huu unafanyika chini ya kaulimbiu ya "kujenga upya uaminifu na kuamsha mshikamano wa kimataifa: Kuharakisha hatua kuelekea Ajenda ya 2030 na Malengo yake ya Maendeleo Endelevu kuelekea amani, ustawi, maendeleo na uendelevu kwa wote". Msururu wa majadiliano baina ya nchi na nchi pia utafanyika kando ya mkutano huo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akitoa tamko wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kilele wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, katika makao makuu wa Umoja wa Mataifa, New York, Marekani, Septemba 18, 2023.Picha: Mike Segar/REUTERS

Jukumu la jumla la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni lipi?

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lenye nchi wanachama 193 linajadili masuala ya haki za binadamu, sheria za kimataifa na ushirikiano katika "nyanja za kiuchumi, kijamii, kitamaduni, elimu na afya". Lina uwezo wa kupitisha maazimio na matamko yanayokusudiwa kuweka kanuni elekezi za shirika hilo.

Kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, chombo hicho pia kina jukumu la kushughulikia masuala ya amani na usalama wa kimataifa ambayo hayashughulikiwi kwa sasa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).

UNGA inaidhinisha bajeti ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa na moja ya kamati zake kuu sita inasimamia moja kwa moja ufadhili wa jumbe za kulinda amani duniani kote.

Nani atazungumza kwenye Mjadala Mkuu?

Rais wa UNGA kwa kawaida hutoa hotuba ya kwanza ya Mjadala Mkuu. Kiongozi wa kikao hiki, Dennis Francis kutoka Trinidad na Tobago, amesema kwamba anataka kutanguliza ushirikiano mkubwa wa kimataifa na fursa sawa wakati wa uongozi wake.

Brazil basi kitamaduni hutoa hotuba ya kwanza ya nchi, huku Rais Luiz Inacio Lula da Silva akitarajiwa kuyafanya mabadiliko ya tabianchi kuwa kiini cha hotuba yake.

Lula, ambaye alichukua wadhifa huo mwezi Januari, ameapa kuirejesha Brazil kama kiongozi wa kimataifa katika uhifadhi wa mazingira na kuimarisha ulinzi wa msitu muhimu wa Amazon baada ya uharibifu wa miaka mingi.

Soma pia: Maelfu waandamana New York kuhimiza mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Marekani, kama nchi mwenyeji, itaifuata Brazil, huku Rais Joe Biden akitarajiwa kutoa hotuba kwenye Baraza Kuu siku ya Jumanne akitafuta kusisitiza nafasi ya Washington kama kiongozi wa kimataifa.

Rais wa Marekani Joe Biden atahutubia UNGA Jumanne, Septemba 19, 2023, akitafuta kutilia mkazo nafasi ya Marekani kama taifa lenye nguvu zaidi duniani.Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Kuanzia hapo, "utaratibu wa wasemaji hufuata kanuni tata inayoonyesha kiwango cha uwakilishi, usawa wa kijiografia, utaratibu ambamo ombi la kuzungumza lilisajiliwa, na mambo mengine ya kuzingatia", Umoja wa Mataifa unasema kwenye tovuti yake.

Viongozi gani wengine watakuwepo?

Takriban viongozi 150 wanatarajiwa kuhudhuria mazungumzo hayo ya ngazi ya juu, ambapo mjadala mkuu unagusia masuala mbalimbali yenye maslahi ya kikanda na kimataifa.

Miongoni mwa wengine, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy atakuwepo, pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Wote wawili wanatarajiwa kuhutubia Baraza Kuu na kufanya mazungumzo na Biden kando ya tukio hilo.

Shirika la habari la Reuters pia liliripoti wiki iliyopita kwamba Zelenskiy atazungumza Jumatano katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Ukraine, jambo ambalo "linaweza kumweka kwenye meza moja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov" huku kukiwa na mashambulizi ya kijeshi ya Urusi.

Nani hatakuwepo?

Biden atakuwa kiongozi pekee wa juu wa nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zenye kura ya turufu - Marekani, China, Urusi, Ufaransa na Uingereza - kuhudhuria wiki hiyo ya ngazi ya juu, vyombo vya habari vimeripoti.

Soma pia: Baraza kuu la UN laitaka Urusi kuondoa majeshi yake Ukraine

Rishi Sunak atakuwa waziri mkuu wa kwanza wa Uingereza katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja kuruka tukio hilo, akisema kuwa ratiba yake yenye shughuli nyingi inamzuia kwenda New York. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia atakosa hafla hiyo, akitoa sababu ya ratiba zinazopishana.

Bado haijafahamika wazi  ni ofisa gani wa China atahudhuria mkutano huo baada ya gazeti la Wall Street Journal kuripoti mapema Septemba kwamba Beijing ilipanga kumtuma Makamu wa Rais Han Zheng badala ya kumtuma Waziri wa Mambo ya Nje Wang Yi katika safari ya Marekani kama ilivyoashiriwa hapo awali.

Baraza kuu la UN lamalizika

01:03

This browser does not support the video element.

Ni mada gani zitajadiliwa?

Kwa kuzingatia utofauti wa wazungumzaji, Mjadala Mkuu kwa kawaida hushughulikia masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa.

Mada kuu za mwaka jana ni pamoja na juhudi za kupona kutokana na janga la COVID-19, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, na mabadiliko ya hali ya hewa - yote ambayo yanatarajiwa kujitokeza tena wakati wa mkusanyiko wa mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa Agosti, mwakilishi wa Marekani, Thomas-Greenfield, alisema anatarajia nchi nyingi za Magharibi kutoa "shinikizo kubwa" kwa Urusi kuondoa wanajeshi kutoka nchi jirani ya Ukraine.

Uvamizi huo umeibua upya wito wa kupanua mamlaka ya kufanya maamuzi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15, ambapo Urusi ni miongoni mwa wanachama watano wa kudumu - pamoja na China, Ufaransa, Uingereza na Marekani - ambao wana mamlaka ya kura ya turufu.

Wasiwasi juu ya China, usalama wa baharini katika kanda ya Pasifiki, usumbufu wa usambazaji na haki za binadamu pia huenda vikaibuka, hasa kwa sababu waangalizi wengine wametilia shaka ushawishi unaokua wa Beijing katika UN.

Soma pia: Maendeleo endelevu yapata ufadhili

Mapinduzi ya hivi karibuni barani Afrika, hasa nchini Niger, yanaweza pia kuzingatiwa zaidi, kama ilivyo kwa vita vinavyoendelea nchini Sudan na Ethiopia. Wakati huo huo, mizozo ya kibinadamu inayoendelea katika maeneo kama vile Afghanistan, Pembe ya Afrika na Amerika Kusini - na jukumu lao katika mzozo wa uhamiaji wa kimataifa - pia inaweza kujitokeza sana.

Wakati huo huo, Mjadala Mkuu unakuja miezi miwili kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi, COP28, utakaofanyika Dubai na Guterres, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, atakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Matarajio ya Hali ya Hewa kando ya tukio la wiki hii huko mjini York.

"Wito wangu kwa viongozi wa ulimwengu utakuwa wazi: Huu sio wakati wa kutangaza au kuweka nafasi. Huu sio wakati wa kutojali au kutokuwa na maamuzi. Huu ni wakati wa kukusanyika pamoja kwa ajili ya suluhu za kweli na za vitendo,” Guterres alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari Septemba 13.

Jinsi kampuni ya mpira inaboresha maisha ya walemavu Kenya

01:35

This browser does not support the video element.

Ni nini nyuma ya mada ya mwaka huu?

Mada zinazotolewa na marais wa UNGA kwa kawaida ni pana - na ya mwaka huu pia.

Francis alisema katika barua ya Juni kwa mtangulizi wake kwamba mada ya 2023 "inajumuisha utambuzi kwamba tuko kwenye njia panda katika historia na kwamba njia iliyo mbele itakuwa muhimu katika kuamua sio tu mustakabali wetu, lakini ule wa vizazi vijavyo".

Alitoa wito wa ahadi mpya kwa ushirikiano wa kimataifa na kuyahimiza mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa  kuangalia namna yanavyoweza kuchukuwa hatua za pamoja kukuza amani na usalama, kupambana dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kukuza haki za binadamu.
Kaulimbiu pia inasisitiza haja ya kuongeza kasi katika juhudi za kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Ni nini Malengo ya Maendeleo Endelevu?

Umoja wa Mataifa umeyataja Malengo ya Maendeleo Endelevu kuwa "wito wa dharura wa hatua" kati ya mataifa kushughulikia umaskini, njaa na masuala mengine ya kimataifa.

Yaliainishwa katika kile kinachoitwa "Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu," iliyopitishwa mwaka 2015 kutoa muongozo wa kutimiza mambo kadhaa kufikia mwaka 2030.

Orodho hiyo inajumlisha malengo 17, ikiwemo kuhakikisha elimu bora, utoaji wa maji safi na usafi, na kuchukuwa hatua za dharura kukabiliana na mzozo wa mabadiliko ya tabianchi.