1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNGA yaidhinisha waraka wa mataifa mawili kumaliza vita Gaza

12 Septemba 2025

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha waraka unaotaka suluhisho la mataifa mawili kwa vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza, pamoja na kukomeshwa kwa utawala wa Hamas katika eneo hilo lililoharibiwa na vita.

Marekani New York 2024 | Benjamin Netanyahu katika Mkutano Mkuu wa 79 wa Umoja wa Mataifa
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza wakati wa Kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Septemba 27, 2024.Picha: Charly Triballeau/AFP/Getty Images

Kura hiyo ilifanyika kabla ya mkutano kuhusu suala hilo utakaofanyika tarehe 22 Septemba, na kabla ya Mjadala Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambapo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametangaza kuwa nchi yake itatambua rasmi Palestina kama taifa.

Hiki ilikuwa kikao cha pili cha Baraza Kuu la umoja huo na mchakato wa kwanza wa zoezi la kupiga kura chini ya uongozi wa rais mpya, ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock.

Waraka huo unasema

"Katika muktadha wa kumaliza vita vya Gaza, Hamas inapaswa kumaliza utawala wake Gaza na kukabidhi silaha zake kwa Mamlaka ya Palestina, kwa ushirikiano na msaada wa kimataifa.”

Mwanamke mtu mzima akiwatazama Wapalestina wakitoa vitu kutoka kwa vifusi vya jengo lililoharibiwa kufuatia mashambulizi ya usiku ya jeshi la Israel kwenye kambi ya al-Shati kwa ajili ya wakimbizi wa Kipalestina, magharibi mwa Gaza City, Septemba 12, 2025Picha: Omar Al-Qattaa/AFP/Getty Images

Waraka huo pia unalaani shambulizi la Hamas dhidi ya Israel la tarehe 7 Oktoba 2023. Waraka wa kurasa saba unaojulikana kama "Azimo la New York" uliandaliwa mwishoni mwa Julai katika mkutano wa Umoja wa Mataifa ulioandaliwa na Ufaransa na Saudi Arabia.

Wakati huo, nchi 17 zikiwemoUingereza, Kanada, Brazil na Jordan zilisaini waraka huo. Israel na mshirika wake wa karibu Marekani waligomea mkutano huo na kuukosoa vikali.

Israel imelikataa azimio hilo

Israel imelaani vikali kura ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa iliyopigwa Ijumaa, ambayo inaunga mkono kuundwa kwa taifa la Palestina lisilo na Hamas, ikisema kuwa hatua hiyo "ni ya aibu” na inaweza kuhamasisha kundi la Hamas kuendeleza vita vya Gaza.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, Oren Marmorstein, alisema kupitia mtandao wa X (zamani Twitter) kuwa Israel "inakata kabisa” azimio hilo, akilitaja kama ushahidi kwamba Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limegeuka kuwa ‘sarakasi ya kisiasa isiyohusiana na uhalisia'.

Waraka huo unapaswa kueleweka kama ramani ya njia ya kutatua mgogoro wa Mashariki ya Kati, kwa misingi ya kuwepo kwa mataifa mawili yanayoishi kwa amani  Israel na Palestina.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW