1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza Kuu la UN kuamua kuhusu ushiriki mpana wa Palestina

10 Mei 2024

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linatazamiwa leo Ijumaa kuipigia kura rasimu ya azimio ambalo huenda litaipatia Palestina uwakilishi mkubwa na haki zaidi ya ushiriki katika vikao vya Baraza hilo.

Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: KENA BETANCUR/AFP/Getty Images

Ikiwa rasimu hiyo ambayo imewasilishwa na Umoja wa Falme za Kiarabu lakini ikaandaliwa na Wapalestina wenyewe itapitishwa, itaipatia Palestina haki zaidi ya kushiriki katika vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lakini haitoipatia haki ya kupiga kura mara kwa mara katika chombo hicho muhimu.

Rasimu hiyo ambayo imekua chanzo cha msuguano kwa wiki kadhaa, inalenga pia kutoa wito kwa Baraza la Usalama, kuzingatia upya ombi la Palestina la kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.

Soma zaidi: Je, Palestina inayotambulika itasaidia kumaliza mzozo wa Gaza?

Itakumbukwa kuwa, mwezi uliopita, rasimu kama hiyo ambayo ingeiwezesha Palestina kutambuliwa kama mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa ilizuiwa na Marekani kwenye Baraza la Usalama la umoja huo.

Naibu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Robert Wood Picha: Yuki Iwamura/AP/picture alliance

Naibu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Robert Wood amesema jana kwamba Washington inapinga kikao hicho cha Baraza Kuu, akiongeza kuwa njia pekee ya kupata uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ni kupitia mazungumzo na Israel.

Mwaka 2012,  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliipatia Palestina hadhi ya uangalizi licha ya upinzani kutoka Marekani. Palestina na Vatican ndio mataifa mawili pekee ambayo si wanachama kamili wa Baraza hilo lakini wenye hadhi hiyo ya uangalizi inayowapa nafasi ya kuhudhuria vikao vya Umoja wa Mataifa bila ya kuwa na haki ya kupiga kura.

Mataifa kadhaa ya EU kulitambua taifa la Palestina

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep BorrellPicha: Press Office, Albania Premiership

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amefahamisha usiku wa jana Alhamisi kwamba mataifa ya Uhispania, Ireland na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya, zinapanga kulitambua taifa la Palestina ifikapo Mei 21 mwaka huu.

Soma zaidi: Uhispania kuitambua Palestina kama taifa huru

Mwezi Machi, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alisema Uhispania, Ireland, Slovenia na Malta, waliafiki kwa pamoja kuchukua hatua za kwanza kuelekea kulitambuliwa taifa la Palestina katika dhamira ya kusisitiza kuwa suluhisho la mataifa mawili ni muhimu ili kufikia amani ya kudumu.

Israel yaendelea kuishambulia Gaza

Huko Gaza kwenyewe, mashambulizi ya Israel yameendelea kushuhudiwa na kusababisha maafa, kama anavyoeleza Saed al-Malah aliyelazimika kuyahama makazi yake:

Moshi ukifuka kufuatia mashambulizi ya mabomu katika mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza: 06.05.2024Picha: AFP/Getty Images

"Tulikuwa tumelala vizuri tu ndipo tukasikia mlipuko mkubwa, kombora lilianguka karibu na hema na kumuua mume wa binti yangu. Ndivyo ilivyokuwa, hakukuwa na wapiganaji wala wanachama wa Hamas. Gaza yote inalengwa na ni kama Israel hawataki kupata suluhisho, wanataka waiharibu nchi nzima."

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa zaidi ya Wapalestina 100,000 wameukimbia mji wa kusini mwa Ukanda huo wa Rafah ambako pia shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto  UNICEF limeonya kwamba akiba ya chakula inaweza kumalizika kabisa katika siku zijazo na kutoa wito wa kuokoa maisha ya watoto eneo hilo.

Soma pia: Israel yaanza kuwahamisha raia 100,000 kutoka Rafah

Katika hatua nyingine, Misri ambayo imekuwa mpatanishi katika mzozo huu uliodumu miezi saba, imezitaka Israel na Palestina kuwa na utashi wa kulegeza misimo yao ili hatimaye waweze kufikia makubaliano ya usitishwaji mapigano na kubadilishana mateka na wafungwa. Kauli hiyo ya Misri imetolewa baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Sameh Shoukry kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na wenzake wa Marekani Antony Blinken.

(Vyanzo: Mashirika)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW