1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMamlaka ya Palestina

Baraza Kuu la UN laidhinisha ombi la uanachama wa Palestina

11 Mei 2024

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo Ijumaa lilipitisha kwa wingi mkubwa wa kura azimio linalounga mkono Palestina kuwa mwanachama kamili wa umoja huo.

Marekani | Kikao maalum cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa | Ombi la Palestina kuwa mwanachama kamili | 
Kikao maalum cha Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: Charly Triballeau/AFP/Getty Images

Azimio hilo limeitambua Palestina kuwa na hadhi ya kupata uanachama kamili na linatoa mwito kwa Baraza la  Usalama la Umoja wa Mataifa "kuunga mkono" azma ya Palestina ya kupata kiti ndani ya Umoja wa Mataifa.

Baraza hilo Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio hilo kwa kura 143 huku 9 zikipinga azimio hilo na 25 wakikosa kushiriki kura hiyo kwa kutokuwepo kwenye kikao hicho. Kura hiyo pia inaitambua haki ya Palestina kuwa mwanachama wa 194 wa Umoja wa Mataifa.

Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyadh MansourPicha: Charly Triballeau/AFP/Getty Images

Marekani kupinga azimio hilo kwa kura ya turufu

Hii inamaanisha kwamba ombi la uanachama wa Palestina litawasilishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ombi la Palestina kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa lililowasilishwa mbele ya Baraza la Usalama mwezi uliopita, lilipingwa na Marekani kwa kura ya turufu, licha ya kuungwa mkono pakubwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Marekani inatarajiwa kurudia kulipinga ombi hilo jipya kwa kura ya turufu.

Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Robert Wood, amethibitisha msimamo huo akisema, utawala wa Rais Biden, unalipinga azimio hilo lililopitishwa.

Endapo Palestina itakuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa, basi umoja huo utakuwa umekiri uwepo wa taifa la Palestina, jambo ambalo Israel, mwandani wa Marekani, imekuwa ikipambana lisifanyike.

Palestina imekuwa mtazamaji tu katika Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2012 kwani haina haki ya kupiga kura.

Usitishwaji wa mapigano Gaza

Katika miaka iliyopita, baadhi ya mataifa yamekerwa na ombi hilo la Palestina, yakisema kwamba taifa lolote linalotaka kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa linastahili kuwa "taifa linalopenda amani."

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Gilad ErdanPicha: Charly Triballeau/AFP/Getty Images

Hali inayoendelea katika maeneo ya mipaka ya Palestina na hasa Gaza, ambapo zaidi ya watu 34,000 wameuwawa tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi yake ya kulipiza kisasi kutokana na shambulizi la Oktoba 7 lililofanywa na wanamgambo wa Hamas, ni hali ambayo imelighadhabisha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo limetoa wito wa usitishwaji wa mapigano.

Hamas kundi ambalo linatambuliwa na Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine kama kundi la kigaidi, limeitawala Gaza tangu mwaka 2007. Ukingo wa Magharibi uliokaliwa na Israel, unatawaliwa na Mamlaka ya Palestina, ambayo ni hasimu wa Hamas.

Chanzo: DW: https://www.dw.com/en/un-general-assembly-approves-palestinian-membership-bid/a-69048032

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW