1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yatoa wito wa mshikamano kukabili vita, njaa na tabianchi

30 Septemba 2025

Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umekamilika kwa wito wa pamoja, kushughulikia changamoto kubwa zinazoukabili ulimwengu, ikiwemo vita vinavyozidi kuongezeka, njaa kali, na ukatili wa kijinsia.

New York 2025 | Annalena Baerbock katika kuadhimisha miaka 80 ya Umoja wa Mataifa
Annalena Baerbock awashukuru viongozi kwa kuonesha moyo wa kuchukua hatua, kukumbatia diplomasia, kutokwepa masuala nyeti wakati wa mkutano wa UNGA:Picha: Eduardo Munoz/REUTERS

Katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo, Rais wa Baraza Kuu Annalena Baerbock alieleza kuwa mataifa wanachama 189 yalishiriki katika Mjadala Mkuu, uliojumuisha viongozi 124 wa nchi na serikali.

Baerbock alitaja kuwa masuala ya amani na usalama yalikuwa mada kuu zilizojitokeza katika hotuba nyingi, huku ujumbe wa pamoja ukiwa wazi kwamba mataifa yanapaswa kuchukua hatua zaidi kuzuia vita na vurugu.

Aliwashukuru viongozi kwa kuonesha moyo wa kuchukua hatua, kukumbatia diplomasia, kutokwepa masuala nyeti, na kwa kuthibitisha kwa nini Umoja wa Mataifa bado ni muhimu hasa wanapokabiliwa na wakati wa maamuzi muhimu.

"Katika kipindi chote cha wiki, mada fulani zilisikika zaidi ya nyingine. Kuu kati ya hizo ni amani na usalama – Gaza, Ukraine, Sudan na maeneo mengine mengi yaliyosahaulika. Ujumbe ulikuwa wazi: nchi wanachama lazima zifanye zaidi kuzuia wimbi la vita na ghasia, kuwalinda na kuwalisha raia wanaokufa njaa huko Gaza, kurejesha amani Ukraine, na kuwalinda wanawake na wasichana nchini Sudan."

"Taasisi hii ni imara kama vile nia yetu ya pamoja ya kutekeleza misingi ya mkataba wetu na sheria za kimataifa. Na tunapofanya hivyo, maendeleo hufuata.”

Mataifa tajiri yahangaika kutimiza ahadi

Rais wa Ghana John Dramani Mahama akihutubia Mkutano Mkuu wa 80 wa Umoja wa Mataifa (UNGA), kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani:Picha: Jeenah Moon/REUTERS

Huku haya yakijiri, viongozi wa nchi zinazoendelea zinazokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi walishtumu mataifa tajiri katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kutotimiza ahadi zao za kufadhili hatua za kukabiliana na kuongezeka kwa kina cha bahari, ukame na ukataji miti.

Mataifa tajiri yamekuwa yakihangaika kutimiza ahadi za ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi. Kiwango cha ufadhili kilifikia dola bilioni 100 kwa mwaka, kiwango kilichokubaliwa mwaka 2009, lakini kilichelewa hadi 2022.

Katika hotuba yake kwa Baraza Kuu wiki iliyopita, rais wa Marekani Donald Trump alipuuzilia mbali mabadiliko ya tabianchi akiyaita "utapeli mkubwa zaidi duniani.” Kauli hii inajiri baada ya rais huyo kuindoa Marekani kwa mara ya pili kutoka mkataba wa Paris na kusitisha ahadi nyingi za ufadhili wa tabianchi.

Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, alisema mabadiliko ya tabianchi "yanalazimisha serikali za nchi zinazoendelea kufanya maamuzi magumu ya kifedha yanayozuia matarajio ya kuwekeza katika ustawi na maendeleo."

Mohamud ameongeza kuwa ukame, mafuriko na kuongezeka kwa kina cha bahari vinaharibu maisha na kuhamisha familia, na kuhatarisha maendeleo ya amani na ustawi. Takriban asilimia 10 ya bajeti za nchi zinazoendelea hutumika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, ahadi zianendelea kutolewa; China, ambayo pia ni mzalishaji mkubwa wa gesi chafu, imeahidi kwamba kufikia mwaka 2035 itapunguza uzalishaji. Kauli hiyo, iliyotolewa na Rais wa China Xi Jinping ilipokelewa kwa ukosoaji na mkuu wa masuala ya tabianchi wa Umoja wa Ulaya ambaye alisema mpango huo "haukidhi kile wanachoamini kinawezekana na kinahitajika."

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW