1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Biashara laingilia mzozo Kenya, Uganda

16 Desemba 2021

Baraza la Biashara la Jumuiya ya Afrika Mashariki limetoa wito wa kutafuta suluhu ya mzozo wa kibiashara  baina ya Uganda na Kenya, likisema mzozo huo umechangia kupunguza biashara kwa 15% katika nchi za jumuiya hiyo.

Afrika Kenia Fischer Markt Hafen
Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza hilo, John Bosco Kalisa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mjini Arusha kwamba mgogoro unaoshuhudiwa sasa baina ya Kenya na Uganda unachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu biashara ya ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuharibu ajira za watu na kuchochea visasi baina ya nchi wanachama.

"Hivi karibuni baraza la mawaziri la Uganda liliazimia kupiga marufuku baadhi ya bidhaa za Kenya kama hatua ya kulipiza kisasi maamuzi ya nchi hiyo jirani, ambayo ilipiga marufuku bidhaa za kuku kutoka Uganda. Mgogoro huo ulianza baada ya wizara ya kilimo ya Kenya kuziandikia mamlaka za mipakani ikiagiza kutoruhusu bidhaa za kuku ikiwemo ya mayai kutoka Uganda kuingizwa Kenya. Hali hiyo imekuwa ikileta uharibifu wa bidhaa baina ya mataifa hayo mawili na nchi zote za jumuiya kwa ujumla.''

Itifaki za Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja za jumuiya hiyo, pamoja na mambo mengine, inahimiza kutowekwa vikwazo vya ushuru kwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya jumuiya hiyo, na hivyo Kalisa anasema mgogoro wa kibiashara unakiukia itifaki hizo.
 
Mkurugenzi huyo alisema Baraza la Biashara la Afrika Mashariki linatoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vyote vya kibiashara hasa usafirishaji wa bidhaa maeneo ya mipakani baina ya nchi wanachama, likisema ushuru unazuia kuwepo kwa soko huru la bidhaa zinazozalishwa ndani ya jumuiya hiyo.

Imeandikwa na Veronica Natalis, DW Arusha