1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa kuchunguza ukiukaji wa haki Afghanistan

6 Oktoba 2025

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeanzisha uchunguzi wa ukiukaji wa haki za binadamu nchini Afghanistan, likilenga hasa mateso ya wanawake na wasichana chini ya utawala wa Taliban unaokosolewa kimataifa.

Picha ya Farzana Wahidy — Wanawake nchini Afghanistan.
Jumuiya ya kimataifa inaushtumu utawala wa Taliban kwa ukandamizaji wa haki za wanawake na wasichana.Picha: AP

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeamua kuanzisha uchunguzi maalum kuhusu ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Afghanistan, hatua inayokuja wakati hofu ikiongezeka juu ya sera kali za watawala wa kundi la Taliban dhidi ya wanawake na wasichana.

Baraza hilo lenye nchi wanachama 47 lilipitisha azimio hilo mjini Geneva bila kupiga kura, likiongozwa na Umoja wa Ulaya (EU).

Lengo ni kukusanya na kuhifadhi ushahidi wa uhalifu wa kimataifa unaotekelezwa nchini humo tangu Taliban ilipotwaa madaraka kwa nguvu miaka minne iliyopita.

Balozi wa Denmark Ib Petersen, akiwasilisha azimio kwa niaba ya EU, alisema hali ya haki za binadamu nchini Afghanistan "imezidi kuwa mbaya katikati ya mgogoro wa kibinadamu unaoendelea.”

Petersen aliongeza kuwa Taliban imeimarisha utawala wa ukandamizaji na kuangamiza kabisa nafasi ya kiraia nchini humo, akisisitiza kuwa "baraza hili lina wajibu wa kusimama kidete na watu wa Afghanistan.”

Wanawake wa Afghanistan wanaelezwa kukabiliwa na ukandamizaji mkubwa chini ya utawala wa Taliban.Picha: Alain Pitton/NurPhoto/picture alliance

Uchunguzi kujikita kwa ukiukaji dhidi ya wanawake na wasichana

Azimio hilo linaunda tume huru ya kimataifa ya uchunguzi yenye jukumu la kukusanya, kuhifadhi na kuchambua ushahidi wa uhalifu mkubwa wa kimataifa na ukiukaji wa sheria za kimataifa, ikiwemo yale yanayohusu wanawake na wasichana.

Tume hiyo pia itaandaa majalada yatakayowezesha kufikishwa kwa kesi huru za jinai, na kuhifadhi simulizi na ushuhuda wa waathiriwa.

Msemaji wa EU aliiambia AFP kwamba chombo hicho kitahakikisha "hadithi za waathiriwa hazipotei bali zinakuwa sehemu ya ushahidi wa kimataifa.”

Tangu Taliban kurejea madarakani mwaka 2021, serikali yake imeendelea kutengwa kimataifa kutokana na sera zake za ukandamizaji, hasa dhidi ya wanawake.

Wanawake wamezuiwa kufanya kazi nyingi, kusafiri bila msimamizi wa kiume, kusoma baada ya umri wa miaka 12, au hata kutembea bustanini na kwenda mazoezini.

Taliban yashutumiwa kwa ubaguzi na udhalilishaji wa kijinsia

Azimio la Baraza la UN linashutumu hatua ya Taliban ya "kuhalalisha mfumo wa ubaguzi, utengano, utawala wa kijinsia na udhalilishaji wa utu wa wanawake.”

Balozi wa Colombia Gustavo Gallon alisema wanawake na wasichana wa Afghanistan "wanakabiliwa na ukandamizaji uliopangwa unaolenga kuwaondoa kabisa katika maisha ya umma.”

Aliendelea kusema kuwa wananchi wote wa Afghanistan "wanateseka katika mazingira ya njaa, ukimbizi na ukandamizaji.”

Wanawake Afghanistan wajitokeza hadharani

01:05

This browser does not support the video element.

Hata hivyo, licha ya kukubali azimio hilo bila upinzani wa moja kwa moja, China ilijitenga na uamuzi huo, ikisema haukutambua hatua chanya zilizopigwa na serikali ya Taliban.

Mwakilishi wa China alisema Afghanistan "imechukua hatua kadhaa za kuimarisha uthabiti, ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.”

Mashirika ya haki za binadamu: Hatua ya kihistoria

Mtafiti wa Afghanistan katika shirika la Human Rights Watch, Fereshta Abbasi, alisema uamuzi wa Baraza la Haki za Binadamu la UN ni "hatua ya kihistoria” kwani unaweka wazi kuwa "wale wote wanaohusika na uhalifu wa zamani na wa sasa watawajibishwa.”

Abbasi aliongeza kuwa uchunguzi huu "unatuma ujumbe kwa Taliban na wahalifu wengine kwamba ushahidi unakusanywa na siku moja watafikishwa mbele ya haki.”

Afghanistan inaelezwa kama moja ya nchi zinazokabiliwa na mgogoro mkubwa wa haki za binadamu duniani, huku matumaini ya mabadiliko yakiwa madogo chini ya utawala wa Taliban unaoendelea kudhibiti kila nyanja ya maisha ya kijamii.

Chanzo: AFP, RTRE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW