1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la haki za binadamu laijadili Syria

29 Aprili 2011

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa leo limeanza vikao maalumu juu ya Syria, huku shinikizo likiongezwa kwa ajili ya kulaani hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya waandamanaji na kutaka kufanyike uchunguzi.

Rais wa Syria Bashar AssadPicha: picture-alliance/dpa

Mjadala huo umeanza kufuatia ombi la mataifa 10 ya Ulaya, Marekani, Mexico, Korea kusini Senegal na Zambia.

Lakini, hata hivyo, wanakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa washirika wa Syria, ikiwemo Urusi na China.

Muswada wa awali uliowasilishwa na Marekani unatoa wito kwa wanachama 47 wa baraza hilo kukubali kuundwe kwa tume huru ya kimataifa ya uchunguzi kwa ajili ya kuchunguza madai yote ya vitendo vya uvunjwaji wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.

Aidha wanadiplomasia kutoka katika nchi za Ulaya na Marekani wamelisisitiza pia Rais Bashar al Assad aruhusu waandishi wa habari wa kigeni na kupunguza vikwazo vya matumizi ya Internet.

Wanadiplomasia hao wamesema dunia inataka kupata picha halisi jinsi utawala wa Syria unavyotumia nguvu kuweza kuwazima waandamanaji hao.

Awali katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, aliunga mkono wito wa Kamishna wa Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa mataifa, Navi Pillay, la kutaka kufanyika uchunguzi nchini Syria juu ya hatua kali zinazochukuliwa na Syria dhidi ya waandamanaji.

Katika hatua nyingine wanaharakati nchini Syria wametoa wito wa kuendelea kwa hamasa kubwa na upinzani wao nchi nzima baada ya sala ya Ijumaa ili kuweka shinikizo zaidi kwa Rais Bashar al Assad.

Waandamanaji nchini SyriaPicha: AP
b

Wito huo umetolewa wakati ambao pia Umoja wa Ulaya umekutana mjini Brussels kuzungumzia uwezekano wa kuiwekea Syria vikwazo.

Wito huo wa kufanyika kwa maandamano makubwa hii leo umetolewa katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa Facebook katika ukurasa unaohusu Mapinduzi ya Syria mwaka 2011.

Lakini kwa upande wake, Waziri wa Habari wa Syria, Adnan Mahmud, amesema hatua kali dhidi ya waandamanaji hao zitaendelea kuchukuliwa.

Katika maandamano yaliofanyika Ijumaa iliyopita, zaidi ya watu 100 waliuawa baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi na gesi ya kutoa machozi waandamanaji. Mamia ya watu pia walikamatwa.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp, ap)

Mhariri:Miraji Othman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW