1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Baraza la Katiba Senegal lafuta kura ya kuahirisha uchaguzi

Sylvia Mwehozi
16 Februari 2024

Baraza la Katiba la Senegal limebatilisha tangazo la kuchelewesha uchaguzi wa rais uliokuwa ufanyike mwezi huu likisema kura ya bunge ilikuwa kinyume na katiba.

Macky Sall
Rais wa Senegal Macky SallPicha: RTS/Reuters

Baraza hilo Katiba la Senegal limesema kuwa muswada uliopitishwa na bunge wa kuchelewesha uchaguzi ulikuwa kinyume na katiba, kulingana na nyaraka iliyothibitishwa na chanzo ndani ya taasisi hiyo.

Soma pia: Uchumi wa Senegal kuzorota kutokana na mkwamo wa kisiasa

Aidha, taasisi hiyo ya katiba pia iliwahi kubatilisha agizo la Rais Macky Sall la Februari 3 ambalo lilirekebisha kalenda ya uchaguzi wiki tatu tu kabla ya kupiga kura. Baraza hilo linasema kwamba "ni vigumu kuandaa uchaguzi wa rais katika tarehe iliyopangwa hapo awali" lakini likapendekeza "mamlaka zinazofaa kufanya uchaguzi huo haraka iwezekanavyo."

Machafuko mjini Dakar baada ya tangazo la kuchelewesha uchaguziPicha: Seyllou/AFP

Rais Macky Sall wa Senegal, mapema mwezi huu alitoa tangazo la kuchelewesha uchaguzi ambao awali ulikuwa ufanyike Februari 25. Uamuzi huo umeitumbukiza Senegal katika mzozo mbaya wa kisiasa na kuchochea hasiara kubwa ya umma na maandamano ya vurugu.

Baadae bunge la nchi hiyo liliidhinisha tangazo la kuchelewesha uchaguzi hadi Desemba 15, lakini baada ya vikosi vya usalama kuvamia majengo ya bunge na kuwaondoa baadhi ya wabunge wa upinzani waliokuwa wakipinga muswada.

Kura hiyo ilipisha njia kwa rais Sall, ambaye mamlaka yake ya muhula wa pili yanatarajiwa kumalizika mwezi Aprili, kuweza kusalia mamlakani hadi mrithi wake atakapopatikana, pengine si kabla ya 2025.

Akiwa amekabiliwa na hasira ya umma inayozidi kuongezeka, Rais Sall ameonyesha nia ya kutafuta njia za kupata "maridhiano".

Uamuzi huo wa Baraza la katiba umetolewa wakati wapinzani kadhaa wa serikali waliokuwa wanazuiliwa wakianza kuchiliwa huru kutoka gerezani, katika juhudi zinazoashiria kwamba Rais Sall anatafuta kutuliza hasira ya umma.

Ousmane Sonko, ambaye ni mmoja wa wapinzani wakuu wa Sall, amezuiliwa tangu 2023 lakini hapajakuwa na taarifa za uwezekano wa kuachiliwa kwake.

Wanachama wa makundi ya asasi za kiraia na viongozi wa dini wa Senegal wakizungumza na waandishi wa habariPicha: Seyllou/AFP

Upinzani nchini Senegalumepinga hatua ya Rais Sall ya kuchelewesha uchaguzi ukisema ni "mapinduzi ya kikatiba" na kwamba chama chake kinahofia kushindwa katika sanduku la kura. Uamuzi wa kuahirisha uchaguzi ulichochea maandamano makubwa ambayo hadi sasa yamesababisha watu watatu kupoteza maisha.

Bofya hapa kusoma ripoti hii: Blinken: Uchaguzi ufanyike kama ulivyopangwa Senegal

Washirika wakuu wa kimataifa wa Senegal, pia walilaani hatua hiyo na kutoa wito kwa serikali kufanya uchaguzi haraka iwezekanavyo, kwa hofu ya kutokea ghasia. Upinzani na makundi ya asasi za kiraia yameitisha maandamano mapya leo Ijumaa. Maandamano mengine ya amani yaliyoandaliwa na jumuiya ya asasi za kiraia yamepangwa kufanyika Jumamosi.

Kulingana na baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu, zaidi ya wanachama 1,000 wa upinzani wamekamatwa tangu 2021, wakati Sonko alipoanza mvutano mkali na serikali ambao ulizua machafuko mabaya.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW