1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaidhinisha makubaliano ya kuachiliwa huru mateka

22 Novemba 2023

Israel yaidhinisha makubaliano ya kuachiliwa huru mateka

Israel Tel Aviv Maandamano ya kuishinikiza serikali kuwarudisha nyumbani mateka
Familia na marafiki wa karibu wa watu waliochukuliwa mateka na Hamas waihimiza serikali kuwarudisha nyumbani wapendwa waoPicha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Mkutano huo wa baraza la mawaziri umefanyika baada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuitisha mkutano sawa na huo na baraza lake la mawaziri maalum kwa ajili ya vita na usalama.

Kuelekea kura hiyo ya kuidhinisha makubaliano ambayo yatatoa nafasi ya kuachiliwa kwa baadhi ya mateka, Netanyahu amesema serikali ilikuwa inakabiliwa na uamuzi mgumu, lakini anaunga mkono makubaliano hayo.

Netanyahu ameashiria pia uwezekano wa "kuwepo na habari njema hivi karibuni" juu ya makubaliano ya kuwaachila huru mateka, makubaliano ambayo Marekani imesema yako karibu kuafikiwa.

Soma pia: Ujerumani yahimiza uwajibikaji wa kimataifa ukanda wa Gaza 

Maelezo kamili ya makubaliano hayo bado hayajatolewa rasmi ingawa ripoti za vyombo vya habari zinaashiria kuwa mateka kadhaa huenda wakaachiliwa huru hivi karibuni kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha vita katika ukanda wa Gaza.

Hata hivyo, afisa mmoja wa Marekani ameeleza kuwa, makubaliano hayo yatahusisha mateka 50 waliochukuliwa kutoka Israel, wengi wao wanawake na watoto, na kubadilishana wafungwa 150 wa Palestina pamoja na usitishwaji wa vita kwa siku nne au tano.

Usitishwaji huo wa vita utatoa nafasi ya kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu huko Gaza.

Pendekezo la kuachiliwa mateka liliwasilishwa jana

Familia za mateka waliotekwa na nyara na HamasPicha: Reuters

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Qatar Majed Al-Ansari amesema pendekezo la makubaliano ya kuachiliwa mateka liliwasilishwa kwa Israel mapema jana Jumanne.

Al-Ansari ameongeza kuwa, Qatar inasubiri matokeo ya kura ya baraza la mawaziri la Israel kuhusu pendekezo la kuachiliwa kwa baadhi ya mateka waliotekwa nyara na kundi la wanamgambo la Hamas mnamo Oktoba 7.

Hamas hadi sasa imewaachiliwa mateka wanne pekee, raia wa Marekani Judith Raanan mwenye umri wa miaka 59 na binti yake Natalie Raanan mwenye umri wa miaka 17 pamoja na wanawake wawili raia wa Israel Nurit Cooper mwenye miaka 79 na Yocheved Lifshitz mwenye umri wa miaka 85.

Wakati hayo yakiarifiwa, wabunge nchini Afrika Kusini wamepiga kura ya kuufunga ubalozi wa Israel mjini Pretoria.

Wabunge pia wameihimiza mamlaka nchini humo kukata kwa muda uhusiano wa kidiplomasia na Israel hadi makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza yatakapoafikiwa.

Soma pia:  UN: Wakimbizi wa Kipalestina wanaishi katika mazingira duni

Siku ya Jumatatu, Israel ilimuita nyumbani balozi wake nchini Afrika Kusini kwa kile walichokiita kuwa mashauriano hata kabla ya wabunge kupiga kura.

Watu zaidi ya 500 wadaiwa kuuwawa hospitalini Gaza

01:49

This browser does not support the video element.

Kura hiyo iliyoitishwa na chama cha upinzani, iliungwa mkono na chama tawala cha ANC cha Rais Cyril Ramaphosa. Serikali ya Ramaphosa itakuwa na uamuzi wa mwisho iwapo hatua zilizochukuliwa na bunge zitatekelezwa.

Mapema jana, Rais Cyril Ramaphosa aliandaa mkutano kwa njia ya mtandao na viongozi wenzake wa BRICS kuujadili mzozo kati ya Israel na Kundi la Hamas.

Wakati wa mkutano huo, kiongozi huyo wa Afrika Kusini alikosoa hatua za serikali ya Israel katika mzozo wake na Hamas. Aliishtumu Israel kwa uhalifu wa kivita na kufanya "mauaji ya halaiki" katika ukanda wa Gaza. Israel hata hivyo imekanusha shutma hizo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW