Baraza la mawaziri Misri latangaza kujiuzulu
22 Novemba 2011Katika kauli yake aliyowasilisha kupitia televisheni ya taifa, msemaji wa serikali alisema serikali imekwishwa wasilisha taarifa ya kujiuzulu, lakini itaendelea na majukumu yake ya kila siku nchini humo katika kukabiliana na wakati mgumu.
Hata hivyo kuna taarifa zenye utata juu ya mapokezi ya baraza la kijeshi la nchi hiyo kuhusu taarifa hiyo. Hatua hiyo inafuatia vurugu za siku tatu nchini humo kati ya vikosi vya usalama vya Misri na raia wanaoandamana katika uwanja wa Tahrir.
Zaidi ya watu 20 wameuwawa katika machafuko hayo. Mapema jana wanadiplomasia 140 wa Kimisri waliopo katika wizara za kigeni na balozi nje ya taifa hilo wametoa tamko lililotaka vikosi vya usalama viache kutumia nguvu dhidi ya raia wanaoandamana kwa amani.
Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri: Josephat Charo