1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la mpito Haiti laahidi utulivu na demokrasia

28 Machi 2024

Baraza la mpito nchini Haiti ambalo limepewa jukumu la kusimamia uchaguzi limeahidi kurejesha utulivu na utaratibu wa kidemokrasia kwenye taifa hilo la Karibia ambalo linakabiliwa na ghasia za magenge ya uhalifu.

 Haiti
Polisi nchini Haiti wakiwa kwenye doria katika mitaa ya nchi hiyo inayokabiliwa na ghasia za magenge ya uhalifuPicha: Odelyn Joseph/AP/dpa/picture alliance

      
Baraza la mpito nchini Haiti ambalo limepewa jukumu la kusimamia uchaguzi, limeahidi kurejesha utulivu na utaratibu wa kidemokrasia kwenye taifa hilo la kanda ya Karibia ambalo limeandamwa na wiki kadhaa za ghasia za magenge ya wahalifu yaliomlazimisha Waziri Mkuu Ariel Henri kujiuzulu. 

Soma zaidi. Ufaransa imewahamisha raia wake zaidi ya 170 kutoka Haiti kulikoelemewa na machafuko

Wajumbe nane kati ya kati ya tisa wa Baraza wametoa taarifa inayosema kuwa wamedhamiria kumteua Waziri Mkuu ambaye atasaidia kuirejesha Haiti kwenye demokrasia, utulivu na utu kwa watu kwa taifa hilo ambalo kwa muda mrefu limekabiliwa na ghasia.

Taarifa ya wajumbe hao iliongeza kwa kutoa wito kwa umoja na kusisitiza kuwa nchi hiyo ipo kwenye hatua muhimu ya mabadiliko na kwamba upo mpango wa wazi wa kurejesha utulivu, kufanya uchaguzi huru na kuboresha usalama wa umma nchini humo.

Kwa mujibu wa ripoti ya ainisho ya Awamu ya Usalama wa Chakula ni kwamba karibu nusu ya idadi ya watu nchini Haiti wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakulaPicha: Orlando Barria/EPA

Waziri Mkuu Ariel Henry, ambaye ameiongoza Haiti tangu kuuawa kwa rais Jovenel Moise mwaka wa 2021, aliahidi zaidi ya wiki mbili zilizopita kujiuzulu baada ya baraza la mpito kuundwa ingawa kufikia hatua hiyo imeonekana kuwa ngumu kutokana na tofauti miongoni mwa viongozi wa vyama.

Soma zaidi. Baraza la mpito Haiti lakwama kutokana na tofauti za wajumbe

Baraza tawala la mpito litakalojumuisha wajumbe saba wenye haki ya kupiga kura na wawili wasiopiga kura, lilitangazwa machi 11 baada ya mikutano kadhaa ya dharura kati ya viongozi wa Haiti na mashirika kadhaa ikiwemo jumuiya ya nchi za Karibia CARICOM.

IPC: Nusu ya idadi ya watu Haiti wana uhaba wa chakula

Kwa mujibu wa ripoti ya ainisho ya Awamu ya Usalama wa Chakula IPC ni kwamba takriban watu milioni tano sawa na kusema karibu nusu ya idadi ya watu nchini Haiti wamedumbukia kwenye uhaba mkubwa wa chakula tangu kuongezeka kwa ghasia.

Mkuu wa Shirika la Kimataifa linaloshughulikia watoto Catherine Russell amesema ni muhimu wa kurejeshwa kwa utawala wa kisheria na utaratibu nchini Haiti ili kulinda shule, hospitali na kutoa nafasi ya misaada ya kibinadamu nchini humoPicha: Eduardo Munoz Alvarez/AP/picture alliance

Mkuu wa Shirika la  kimataifa linaloshughulikia watoto, UNICEF, Catherine Russell alitoa wito mwanzoni mwa wiki hii wa kurejeshwa kwa utawala wa kisheria na utaratibu nchini Haiti ili kulinda shule, hospitali na kutoa nafasi ya misaada ya kibinadamu nchini humo.

Soma zaidi. Haiti: Juhudi za kuunda Baraza la mpito zaambulia patupu

Pascal Joseph, ambaye ni mlemavu wa miguu anayeishi katika mji mkuu wa nchi hiyo anasema kwa sasa hali ni mbaya katika mitaa yaHaiti.

 Leo mimi ni dhaifu, najiona mdogo. Ndio ninachoweza kusemasasa hivi, na sio kwamba najisemea tu. Lakini kwa wafanyabiashara wadogo, kwa wafanyabiashara wa simu. Sote tumetawanyika karibu na Champ de Mars. sasa, na hatuna wa kutusaidia. Hatuna mtu wa kutuunga mkono." amesema Pascal Joseph.
 
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya Wahaiti 360,000 wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani na maelfu wameuawa nchini humo ama kwa ghasia, kushindwa kupata msaada wa huduma muhimu kama afya na chakula.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW