Baraza la Mpito la Libya kwenye mtihani
20 Septemba 2011Ni kama kwamba Walibya wanajiona wametoka kwenye mdomo wa chewa na sasa wako huru kutoka mikononi mwa mtu aliyejiita Muangalizi, Kaka Kiongozi na Mfalme wa Wafalme wa Afrika, Muammar Gaddafi.
Ukweli kwamba kumekuwako na sauti nyingi za upinzani na kutokuridhika siku hizi, kunachukuliwa na wachambuzi kwamba si kitisho kwa watawala wapya wa Libya, bali ni dalili kuwa nchi hiyo inafunguka upya kutoka miongo minne ya udikteta wa Gaddafi.
Wale wanaopendelea mfumo wa serikali usioongozwa na dini na wale wanaotaka dini iwe na nafasi muhimu katika uendeshaji nchi hivi sasa wanalumbana juu ya namna bora kabisa ya kuiongoza Libya mpya, huku viongozi wa miji na vijiji walioshiriki kwenye miezi sita ya mapinduzi wakidai nafasi katika serikali mpya.
Hata hivyo, wachambuzi wanaona kuwa ule umoja uliooneshwa na Walibya baada ya wimbi la mageuzi kuanza mjini Benghazi mwezi Februari, hauko hatarini hivi sasa na uungwaji mkono wake kutoka kwa mataifa ya Kiarabu na ya Magharibi uliosaidia kumuangusha Gaddafi bado ni madhubuti.
Badala yake, wachambuzi hao wanasema, kuibuka huku kwa sauti za malalamiko na madai ni matokeo ya kupumua kwa Walibya baada ya kuporomoka kwa dola ya mkono wa chuma chini ya Gaddafi, ambapo sasa sauti yake haitawali tena kwenye redio, televisheni na magazeti.
Katika uwanja wa Mashahidi, ambapo askari wa barabarani aliyevalia sare nadhifu anafanya doria Jumatatu iliyopita kwa mara ya kwanza tangu Gaddafi aondolewe madarakani, mhandisi Mustafa Shaab bin Raghib anataja vipaumbele vyake.
"Kuchelewa kuundwa serikali mpya si jambo muhimu. Ni kama vile mtu anayeumwa, hulazimika kutembea polepole kabla hajaweza tena kutembea kwa mwendo wa kasi. Tunahitaji muda wa kujijenga tena upya", mhandisi huyo ameliambia shirika la habari la Reuters.
Raghib anasema kuwa, si jambo dogo kwamba wameweza kumuondoa yule aliyemuita "kima" akimaanisha Gaddafi, na anaamini kuwa sasa Libya ni bora zaidi kuliko hapo kabla. "Kwanza lazima tumtundike Gaddafi na wanawe wa kiume, kisha tutaweza kupumua kwa uhuru. Bado ni mapema kufanya siasa", ameongeza Raghib.
Maoni haya ni sawa na ya mwalimu mstaafu, Ramadhan Bashiroun, ambaye anasema ni jambo la kawaida kwa watawala wapya kuchukuwa muda kufikia makubaliano. Mwalimu Bashiroun anasema: "Gaddafi alituchoma kwa miaka 40 mizima. Aliuvunja uwezo wetu wote wa kufikiri".
Ustahmilivu huu wa wakaazi wa mji mkuu Tripoli imesaidiwa na kurudi tena kwa huduma za umeme, maji, maduka ya vyakula, mawasiliano na kuanza kutolewa mishahara baada ya miezi kadhaa ya vita.
Lakini subira ina mipaka yake, na viongozi wa Baraza la Mpito wanajua kuwa hatua kubwa ya kijeshi ni muhimu sana kwao. Kushindwa kwa wapiganaji wake kuichukuwa miji ya Bani Walid, Sirte na Sabha inayoshikiliwa na Gaddafu hadi sasa, kunatishia heshima ya Baraza la Mpito.
Jumapili iliyopita, wapiganaji hao walikimbia roho mkononi kutoka mji wa Bani Walid, baada ya kushindwa tena kuuteka. Wapiganaji hao waliliambia shirika la habari la Reuters kuwa kilichowaponza ni kupokea amri zinazopingana kutoka kwa makamanda wao, kutokuwepo kwa sehemu moja ya kutoa maelekezo na vyeo visivyofahamika.
Hadithi kwenye mji wa Sirte inafanana na hii, ambako vikosi vya Baraza la Mpito vimepiga hatua nzuri kidogo, lakini hadi sasa havijaweza kuudhibiti hasa mji huo, vikikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Gaddafi. Yumkini havitaweza kupiga hatua nyengine yoyote bila ya msaada wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO kutoka angani.
Lakini mwanasheria wa Algeria, ambaye aliwahi kuitetea Libya katika kesi ya Lockerbie, Saad Djabbar, anasema kwamba mtafaruku huu si jambo la kushangaza hata kidogo kwa Walibya na lisiwape khofu washirika wao wa kigeni.
Maana ushirika uliomuangusha Gaddafi iliwahusisha Walibya wanaoishi nje, wanaharakati kutoka makundi ya ndani yanayompinga Gaddafi na Walibya wa kawaida kutoka historia na uzoefu tafauti, ambao kitu pekee kilichowaunganisha ni kuteseka kwao chini ya mikono ya Gaddafi.
Djabbar anasema, katika hali kama hii ambapo kila mmoja alijitokeza kwa tangazo la muda mfupi tu, huwezi kutarajia kuwa kila kitu kitakwenda salama usalimini, mia kwa mia.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman