Baraza la Seneti lamkemea Trump kuhusu Saudia na Khashoggi
14 Desemba 2018Ijapokuwa maazimio hayo kwa kiasi kikubwa ni ya kiishara – kwa sababu haijulikani kama yatazingatiwa na baraza la wawakilishi – kupitishwa kwake kunaonesha nia ya maseneta kuisimamia sera ya mambo ya kigeni ya utawala wa Trump na uhusiano wake na Saudi Arabia.
Azimio la kwanza lilipendekeza kuwa Marekani isitishe msaada wake kwa vita vinavyoendeshwa na Saudi Arabia nchini Yemen. Jingine likamtuhumu mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman. Yote mawili yalikuwa yamepingwa vikali na utawala wa Trump, aliyetishia kutumia kura yake kuyapinga. Seneta Bernie Sanders wa VERMONT alielezea kupitishwa kwa maazimio hayo kuwa tukio la kihistoria."Baraza la Seneti limesema kwa sauti kubwa kuwa hatutaendelea kuruhusu hadhi ya jeshi letu kuongozwa na utawala wa kimabavu na wa wauwaji nchini Saudi Arabia. Utawala usioheshimu demokrasia na usioheshimu haki za binaadamu. Utawala ambao hakuna asiyejua kuwa kiongozi wake alihusika katika mauaji ya mwanahabari mkosoaji Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Uturuki".
Ingawa Trump amekuwa akisita kumshutumu bin Salman, akisema kuwa Marekani inanuia kusalia kuwa mshirika imara wa Saudia, kwa azimio hilo Baraza la Seneti linaamini kuwa Mohammed bin Salman ndiye aliyehusika na mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi.
Pia linawataka Wasaudi wamuachie huru Raif Badawi, dada yake Samar Badawi, na wanaharakati wa haki za wanawake nchini Saudi Arabia ambao walikamatwa na kuwekwa ndani kama wafungwa wa kisiasa mwaka huu.
Azimio hilo linasema kuwa uhusiano wa Marekani na Saudi Arabia ni muhimu kwa usalama wa kitaifa wa Marekani na maslahi ya kiuchumi lakini linaitaka Saudia kuitathmini na kurekebisha sera yake ya kigeni.
Maazimio yote mawili yamekuja ikiwa ni miezi miwili baada ya kuuawa mwanahabari huyo wa Saudia katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul na baada ya Trump kila mara kumuondolea lawama bin Salman. Maafisa wa ujasusi wa Marekani walitoa ripoti baada ya uchunguzi wao wakisema kuwa mwanamfalme huyo lazima alifahamu kuhusu njama ya mauaji hayo.
Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Mohammed Khelef