1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la seneti nchini Brazil lambana Bolsonaro

27 Oktoba 2021

Baraza la Seneti la Brazil limependekeza kwamba Rais Jair Bolsonaro anakabiliwa na msururu wa mashitaka ya uhalifu kufuatia hatua zake zinazihusiana na mapambano dhidi ya COVID-19.

Brasilien, Jair Bolsonaro bei einer Videokonferenz zum Thema Coronavirus
Picha: Marcos Corrêa/dpa/Palacio Planalto/picture alliance

Wajumbe 7 wa kamati ya baraza hilo waliunga mkono mapendekezo hayo dhidi ya wajumbe 4 waliopiga kura jana Jumanne. Kamati hiyo kwa miezi sita imekuwa ikichunguza namna serikali ilivyokuwa inalishughulikia janga hilo pamoja na miito ya waendesha mashitaka ya kumshitaki Bolsonaro kwa madai yanayoanzia ulaghai na kuchochea uhalifu hadi matumizi mabaya ya fedha za umma pamoja na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Mashtaka yaliyojadiliwa zaidi miongoni mwa yaliyopendekezwa na kamati hiyo ya seneti ni ya kuchochea janga linalosababisha vifo. Adhabu ya kifungo kwa mtu anayepatikana na kosa kama hilo ni kati ya miaka 20 na 30. Bolsonaro pia anatuhumiwa kwa kukiuka itifaki za afya, kughushi nyaraka za kibinafsi, matumizi mabaya ya fedha za umma, uhalifu dhidi ya binadamu, ukiukwaji wa haki za kijamii na ukiukaji wa maadili ya rais.

Zaidi ya watu 600,000 walikufa baada ya kuambukizwa virusi vya corona nchini Brazil.

Soma Zaidi: Maambukizi ya corona yafikia milioni 4.7 ulimwenguni

Waandamanaji wakiwa katika mitaa ya Rio de Janeiro wakimpinga rais Jair Bolsonaro na serikali yake.Picha: Ricardo Moraes/REUTERS

Bolsonaro mwenyewe anakana madai hayo dhidi yake, huku maseneta wenyewe wakionyesha dhamira thabiti ya kuhakikisha kwamba kiongozi huyo anawajibika, ikiwezekana hata kwa kushirikiana na jumuiya ya kimataifa. Humberto Costa ni mionngoni mwa maseneta hao.

Seneta Humberto Costa aliwaambia waandishi wa habari kwamba "Hatutaishia hapa. Tutakwenda kwa mwanasheria mkuu, kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya haki za binaadamu, tume ya Marekani ya masuala ya haki za binaadamu na mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu. Na juu ya yote, hatutawasahau ama kuwatelekeza wahanga wa COVID-19."  

Bolsonaro akabiliwa na kitisho cha bunge wa kushitakiwa.

Hata hivyo, profesa wa sheria katika chuo kikuu cha Sao Paulo Gustavo Badaro anasema kesi hiyo haina nguvu kwa sababu Bolsonaro hakulianzisha janga hilo. Kulingana na Badaro kesi nzito dhidi ya Bolsonaro kwenye ripoti ya mwisho ni tuhuma ya kuchelewesha au kujitenga na hatua ambazo alitakiwa kuzichukua kama sehemu ya wajibu wake akiwa afisa wa umma, kwa sababu za kibinafsi.

Macho sasa ni kwa mwendesha mashitaka Augusto Aras iwapo ataanzisha uchunguzi dhidi ya swahiba wake rais BolsonaroPicha: Jefferson Rudy /Agência Senado

Adhabu ya mashitaka kama hayo ni kifungo cha kati ya miezi mitatu hadi mwaka mmoja jela. Lakini, kulingana na profesa Badaro, madai kama hayo yanatosha kabisa kumuondoa Bolsonaro mamlakani.

Mwendesha mashitaka mkuu wa Brazil Augusto Aras ambaye huko nyuma alikuwa upande wa Rais Bolsonaro na kuonekana wazi kabisa anamkingia mgongo rais huyo, atatakiwa kuamua iwapo uchunguzi huo wa seneti utamtaka kuanzisha uchunguzi wake. Na baada ya hapo, atatakiwa kupata ruhusa kutoka kwa mahakama ya juu kabisa kuendelea na uchunguzi huo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya uchunguzi Omar Aziz amesema wanataraji kuwasilisha mapendekezo hayo kwa mwendesha mashitaka mkuu hii leo, ingawa hawana matumaini kwamba ataanzisha uchunguzi dhidi ya Bolsonaro.

Uchunguzi huo pia huenda ukachochea Bolsonaro kuanzishiwa mchakato rasmi wa bunge wa kumshitaki ama kuipeleka kesi dhidi yake kwenye mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ya mjini The Hague, ICC.

Mashirika: APE/DPAE