1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la UN lailaani Israel kwa ghasia za Gaza

Daniel Gakuba
14 Juni 2018

 Azimio lililowasilishwa na nchi za Kiarabu kulaani Israel kwa kutumia nguvu za ziada kuzima ghasia na maandamano karibu na mpaka baina yake na Ukanda wa Gaza limepata kura 120 katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

UN-Vollversammlung verurteilt Israel für Gewalt im Gazastreifen
Picha: picture-alliance/Xinhua/Li Muzi

Nchi 120 kati ya 193 wanachama zimeunga mkono azimio hilo ambalo pia limemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupendekeza mkakati wa kimataifa wa kuyalinda maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kimabavu na Israel. Kura nane tu ndizo zililipinga azimio hilo, na nchi 45 zilijizuia kupiga kura.

Azimio hilo lilifikishwa katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa na Algeria, Uturuki na Wapalestina, baada ya Marekani kulizuia kwa kura yake ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mapema mwezi huu.

Azimio hilo pia limelaani kurushwa kwa maroketi kutoka Ukanda wa Gaza hadi maeneo ya raia nchini Israel, lakini halikutaja jina la Hamas, kundi lenye msimamo mkali wa Kiislamu linalotawala katika Ukanda wa Gaza. Ingawa maazimio yanayopitishwa katika baraza kuu hayana uzito kisheria, yana umuhimu mkubwa kisiasa.

Marekani yasimama kando tena

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley amelikosoa azimio hilo akisema linaegemea upande mmoja, kwa kutolitaja kundi la Hamas ambalo amesema ndilo chanzo cha vurugu katika Ukanda wa Gaza. Marekani ilijaribu kulifanyia marekebisho azimio hilo kwa kuingiza kundi la Hamas, lakini juhudi zake ziligonga mwamba.

Riyad Mansour, Balozi wa Palestina katika Umoja wa MataifaPicha: picture alliance/AP Photo

Marekebisho hayo yaliungwa mkono na nchi 62, yakapingwa na nchi 58, huku nyingine 42 zikichagua kutopiga kura kabisa.

Naye balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Danny Danon, amedai kuwa kwa kupitisha azimio hilo,  baraza hilo kuu la Umoja wa Mataifa limeonyesha kula njama na kundi la kigaidi.

Wapalestina zaidi ya 120 waliuawa na vikosi vya usalama vya Israel katika maandamano ya mpakani yaliyoanza tarehe 30 Machi. Idadi kubwa ya wapalestina iliuawa tarehe 14 Mei, siku Marekani ilipouhamisha ubalozi wake kutoka mjini Tel Aviv hadi Jerusalem, hatua ambayo ilisababisha utata mkubwa na kukosolewa na wengi duniani.

Israel yazishutumu nchi ''kula njama na magaidi''

Wakati Israel ikikosolewa vikali kutoka jumuiya ya kimataifa, imejitetea ikisema wengi waliouawa ni wanamgambo, na kwamba maafisa wake walikuwa wakilinda mpaka wao. Marekani muda wote imetetea kile inachokiita ''haki ya Israel kujilinda'' na imeepuka kuungana na wale wanaoikosoa nchi hiyo.

Nikki Haley, Balozi wa Marekani katika Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/ZumaPress/M. Brochstein

Muakilishi wa Wapalestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour amesema wanachokihitaji ni ulinzi wa raia wao, na kutoa hoja kwamba kupitishwa kwa azimio hilo kutasaidia kupunguza mivutano.Mansour amesema na hapa namnukuu, ''Hatuwezi kusalia kimya tukikabiliwa na uhalifu mkubwa unaotumia ghasia na kuvunja haki za binadamu za watu wetu'', mwisho wa kumnukuu.

Azimio hilo la baraza kuu la Umoja wa Mataifa limemtaka Katibu Mkuu Guterres kuwasilisha katika muda wa siku 60, mapendekezo kuhusu njia na namna ya kuhakikisha usalama na ulinzi wa Wapalestina wanaoishi katika maeneo yanayokaliwa kimabavu na Israel.

Desemba mwaka jana, nchi 128 zilikaidi uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump, na kupiga kura katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa, likiitaka Marekani kuacha kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre,ape

Mhariri: Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW