1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

UN yaitaka Israel kukomesha ukaliaji wa maeneo ya Palestina

18 Septemba 2024

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura kwa wingi mkubwa kuitaka Israel kuondoka kwenye maeneo ya Wapalestina inayoyakalia ndani ya mwaka mmoja.

Marekani New York| Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: ANGELA WEISS/AFP/Getty Images

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeunga mkono kwa kiasi kikubwa azimio lisilofungamanisha kisheria la Palestina linaloitaka Israel kuondoka Gaza na maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Ukingo wa Magharibi.

Mataifa 43, zikiwemo Ujerumani, yamejizuwia kupiga kura kuhusu azimio lililowasilishwa katika hadhira kuu ya Umoja wa Mataifa, yenye mataifa wanachama 193.

Soma pia: Vifo vyapindukia 40,000 Gaza

Israel yenyewe, sambamba na Marekani, zilipiga kura ya hapana dhidi ya rasimu ya azimio hilo, pamoja na mataifa mengine 12, huku baadhi ya mataifa yakishindwa kupiga kura.

"Hivi ndivyo siasa za kijinga za kimataifa zinavyoonekana," msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Israel Oren Marmorstein alisema kwenye mtandao wa  X baada ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kupitisha maandishi ya azimio hilo kwa kura 124 dhidi ya 14 huku 43 zikijizuia.

Alisema ni "uamuzi potofu ambao umetenganishwa na ukweli, unahimiza ugaidi na unadhuru fursa za amani".