1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama kujadili mzozo wa Urusi na Ukraine

31 Januari 2022

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana Jumatatu kwa mara ya kwanza kujadili hatua ya Urusi kuitishia Ukraine na kurundika majeshi karibu na mpaka wa nchi hiyo.

USA | UN Sicherheitsrat in New York zur Lage in Äthiopien
Picha: Manuel Elias/Xinhua/picture alliance

Marekani ndiyo iliyotuma ombi la kikao hicho kufanyika na pande zote husika zinatarajiwa kuzungumza hadharani kuhusiana na uwezekano wa Urusi kufanya uvamizi na athari yake kwa dunia.

Alipokuwa akitangaza tarehe ya kufanyika kwa mkutano huo, balozi wa Marekani Linda Thomas-Greenfield amesema hatua ya Urusi ni kitisho cha wazi kwa amani na usalama wa dunia na kanuni za Umoja wa Mataifa.

Balozi wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa Linda Thomas-GreenfieldPicha: Luiz Rampelotto/EuropaNewswire/picture alliance

Bi Thomas-Greenfield amesema wanachama wa baraza hilo ni lazima watazame ukweli na wazingatie athari kwa Ukraine, Urusi na Ulaya iwapo Urusi itaivamia Ukraine.

Urusi kupinga kufanyika kwa mkutano

Urusi kupitia kwa naibu balozi wake katika Umoja wa Mataifa Dmitry Polyansky imeghadhabishwa na hatua hiyo ya Marekani ikiwataka wanachama wa baraza hilo la Umoja wa Mataifa wasiunge mkono ajenda hiyo.

Matamshi haya ya Polyansky yanaashiria kwamba huenda Urusi ikaanza mkutano kwa kuitisha kura ya kupinga kuendelea kwa mkutano huo. Ili kuzuia mkutano usifanyike, Urusi itahitaji kuungwa mkono na wanachama tisa kati ya 15 waliopo.

Thomas Greenfield lakini amesema Baraza hilo la Usalama limeungana na hawatotereka.

"Urusi haiwezi kuzuia mkutano wa Baraza la Usalama kufanyika. Bila shaka watajaribu kutatiza umoja wetu ila wanajua hawawezi kuuzuia mkutano huo, na natarajia hilo ukizingatia kile tunachokijadili. Ila Baraza la Usalama lina umoja. Sauti zetu zimeungana kuitaka Urusi ijieleze," alisema Bi Greenfield.

Uingereza kuipa Ukraine wanajeshi, silaha na meli za kivita

Afisa mmoja mwandamizi katika serikali ya Marekani amesema wanawasiliana mara kwa mara na wanachama wa baraza hilo na wana uhakika kwamba wanaungwa mkono pakubwa ili kuendelea na mkutano huo.

Putin na Biden wakutana

01:15

This browser does not support the video element.

Huku mivutano ikiwa inaongezeka, Marekani inasema iko tayari kukabiliana na taarifa zozote za uongo zitakazotolewa na Urusi katika kile kinachoonekana kuwa kikao cha Umoja wa Mataifa kitakachotazamwa kwa karibu zaidi.

Hayo yakiarifiwa Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnsonnaye ametangaza kwamba wanajiandaa kuupatia muungano wa kujihami wa NATO wanajeshi, silaha, meli na ndege za kivita wakati ambapo waziri huyo mkuu anapotarajiwa kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin wiki ijayo.

Canada nayo Jumapili ilitangaza kuhamishwa kwa muda kwa wafanyakazi wake wasio na majukumu ya lazima kutoka kwenye ubalozi wake mjini Kyiev.

Uhusiano kati ya Urusi na nchi za Magharibi kwa sasa ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu Vita Baridi.

Vyanzo: AFP/AP