Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuijadili Mali
8 Agosti 2012Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana leo kuzungumzia mzozo wa Mali. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, anatarajiwa kutoa taarifa mbele ya baraza hilo, kuangazia wasiwasi wa kimataifa unaozidi kuhusiana na machafuko nchini Mali na mataifa mengine ya Afrika Magharibi.
Kabla kufanyika kikao cha leo cha baraza la usalama, balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Gerard Araud, amesema Ufaransa inatarajia mzozo mrefu nchini Mali, ambako serikali italazimika kufanya harakati ya kijeshi kuyadhibiti maeneo yaliyotekwa na waasi wa kiislamu. Balozi Araud amesema kutakuwa na lazima ya harakati ya kijeshi dhidi ya al Qaeda nchini Mali na kubashiri mchakato mrefu wa kidiplomasia kabla kutumwa tume yoyote ya kulinda amani katika taifa hilo. Kwenye mahojiano yake na televisheni ya Ufaransa, France 24, hapo jana Araud alisema hakuna haja ya kuzungumza na al Qaeda.
Alizitaja hatua za kidiplomasia zinazotakiwa kuchukuliwa kabla baraza la usalama kuridhia kikosi maalumu cha nchi za Afrika, kwa mujibu wa ombi lililowasilishwa na jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS. Jumuiya hiyo imetaka ipewe mamlaka na Umoja wa Mataifa iuende kikosi baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Machi 22 mwaka huu kuzua machafuko yaliyowaruhusu waasi wa Tuareg na wanamgambo wenye mafungamano na al Qaeda kuliteka eneo kubwa la kaskazini mwa Mali.
Araud ambaye ni rais wa baraza la usalama mwezi huu wa Agosti, amesema kwanza serikali ya Mali sharti iombe kikosi hicho halafu baadaye nchi za jumuiya ya ECOWAS lazima zitoe maelezo ya kina juu ya operesheni iliyopendekezwa na baraza hilo. Amesema kuna haja ya kuiimarisha serikali ya Mali na jeshi lake ili iweze kukabiliana na waasi na wanamgambo wa kiislamu.
Mpatanishi wa mzozo wa Mali akutana na waasi
Wakati haya yakiarifiwa, mpatanishi mkuu katika mzozo wa Mali, waziri wa mashauri ya kigeni wa Burkina Faso, Djibril Bassole, amewataka waasi kaskazini mwa Mali wasitishe uhusiano na makundi ya kigaidi kama al Qaeda, kabla mazungumzo ya amani kuanza. Akiwa katika ziara ya kwanza kaskazini mwa Mali, Bassole alikutana jana na kundi la MUJWA katika mji wa Gao na baadaye kwenda katika mji wa Kidal, ambako alikutana na viongozi wa kundi la Ansar Dine lenye mafungamano na al Qaeda.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni baada ya kurejea mjini Ouagadougou, Bassole alisema wanafanya kila wanaloweza kuweka mazingira ya kuzungumza na waasi wa Mali.
Iyad Ag Ghaly, kiongozi wa kundi la waasi la Ansar Dine linaloudhibiti mji wa Kidal, pamoja na miji mingine kaskazini mwa Mali, ameapa kuziunga mkono juhudi za upatanisho kuutanzua mgogoro wa kisiasa ulioigawa Mali. Ghaly aliwaambia waandishi wa habari mjini Kidal baada ya kukutana na waziri Bassole kwamba wako tayari kwa mazungumzo ya amani.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman