Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaiwekea vikwazo vikali Korea Kaskazini
12 Juni 2009Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo linatazamiwa kupitisha azimio la kuiwekea vikwazo vikali zaidi Korea Kaskazini kwa vile nchi hiyo inakataa kuachana na mipango yake ya kuripuwa mabomu ya kinyukliya na kufyetuwa makombora. Baraza hilo linatazamiwa kukutana jioni yal eo na huenda likaupigia kura mswada wa azimio uliokubaliwa na wanachama watano wa kudumu wa baraza hilo ambao wana kura za turufu, Uengereza, China, Ufaransa, Russia na Marekani. Pia Japan na Korea Kusini zimeuunga mkono mswada huo.
Mswada huo unazitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuiwekea vikwazo vikali Korea Kaskazini. Vikwazo hiyvo ni pamoja na kuzikagua meli zinazobeba mizigo inayoshukiwa ina vifaa vilivopigwa marufuku na ambavyo vinahusiana na shughuli za kutengeneza mabomu ya kinyukliya na makombora ya Korea Kaskazini. Pia unataka Korea Kaskazini kunyimwa kusafirishiwa silaha, isipokuwa silaha ndogo ndogo; na pia nchi hiyo iwekewe vikwazo vya mabadilishano ya kifedha.
Ni wazi kwamba mswada huo utakubaliwa, kwani kura tisa zinazounga mkono zinahitajika, lakini kwa sharti kwamba nchi yeyote iliokuwa na kura ya turufu isiupinge mswada huo. Na baada ya mashauriano ya zaidi ya wiki mbili miongoni mwa nchi zilizoupendekeza mswaada huo, yaonesha wazi mswada huo utapitsihwa. Mswada huo unataka kuiadhibu serekali ya Korea Kaskazini kutokana na kitendo chake cha kufanya jaribio la kuripuwa bomu la kinyukliya chini ya ardhi hapo Mei 25 pamoja na baadae kufyetuwa makombora, kinyume na maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice, alisema azimio hilo litapeleka risala kwamba tabia ya Korea Kaskazini haikubaliki. Pia litatoa ishara kwamba Korea Kaskazini lazima iiadhibiwe, irejee bila ya masharti yeyote katika mwenendo wa kufanya mashauriano, ama sivyo itakabiliana na matukeo mabaya.
Mwanzoni mwa mwezi huu, waziri wa ulinzi wa Marekani, Robert Gates, alihakikisha kwamba Korea Kaskazini ilikuwa na nia ya kufanya jaribio la kufyetua roketi la masafa marefu, japokuwa hadi sasa nia ya nchi hiyo sio wazi. Alisema hivi:
" Nimeona baadhi ya ishara kwamba huenda wakafanya kitu, kuyajaribu maroketi mengine ya aina ya TAEPODONG Nambari mbili, lakini hadi sasa sio wazi nini watakachokifanya."
Licha ya malumbano haya, mwakilishi wa Marekani juu ya mzozo wa Korea Kaskazini alielezea matumaini ya kupatikana suluhisho la kidiplomasia pamoja na Korea Kaskazini, na akakisia kwamba nchi hiyo baadae itarejea katika meza ya mashauriano. Mwakilishi huyo, Stephen Bosworth, aliiambia kamati ya Baraza la Senate la nchi yake kwamba serekali ya Marekani inatumia njia mbali mbali kukabiliana na Korea Kaskazini, tangu kuiwekea nchi hiyo vikwazo hadi kushauriana nayo, kidiplomasia, ikiwa nchi hiyo inakusudia kikweli kuifuata njia hiyo. Alisema kwa maslahi ya wale wote wanaohusika, Marekani inatumai kwamba Korea Kaskazini itachaguwa njia ya kidiplomasia badala ile ya mapambano.
Mswada huo unalaani vikali sana jaribio la kuripuwa bomu la kinyukliya lililofanywa na Korea Kaskazini na unaitaka nchi hiyo isifanye majaribio mengine na iachane na kufyetuwa maroketi. Pia nchi hiyo inatakiwa kuachana kabisa na mipango yake yote ya kinyukliya, na jambo hilo lihakikishwe.
Lakini duru za kijasusi za Marekani zimemuonya Rais Barack Obama kwamba Korea Kaskazini inakusudia kulijibu azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kufanya jaribio lengine la kuripuwa bomu la kinyukliya. Inakisiwa kwamba Korea Kaskazini itafanya majaribio matano hadi sita katika juhudi za kuboresha ufundi wake wa kutengeneza mabomu ya kinyukliya.
Japan leo ilisema njia pekee kwa Korea Kaskazini kubakia katika jamii ya kimataifa ni kuambatana na azimio la Umoja wa Mataifa na kuachana na mipango yake ya kinyukliya na ya kufyetuwa maroketi.
Mwandishi:Othman Miraji/AFPE
Mhariri:M.Abdul-Rahman