Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Mzozo wa Syria
1 Februari 2012Wanachama 15 wa baraza la usalama,wengi wao wakiwa mawaziri wa mambo ya nchi za nje walimsikiliza mwakilishi wa jumuia ya nchi za kiarabu akiwasihi wapitishe azimio ili kumaliza "msiba" ulioangamiza maisha ya watu elfu tano tangu mwezi March mwaka jana.
"Hatushauri muingilie kati kijeshi...Hatuungi mkono utawala ubadilishwe,lakini tunapigania shinikizo la kiuchumi" amesema waziri mkuu wa Qatar,Cheikh Hamad ben Jassem Al Thani anaeongoza tume ya jumuia ya nchi za kiarabu kuhusu Syria.Amelalamika kwamba serikali ya Syria haionyeshi moyo wa kutaka kushirikiana kwa dhati,damu inazidi kumwagika na mauwaji yanaendelea.
Wakati baraza la usalama la umoja wa mataifa linaendelea na mjadala wake,nje karibu na jengo la taasisi hiyo muhimu ya kimataifa,wapinzani wa serikali ya Syria wamehanikiza kudai "Syria ikombolewe"
Licha ya miito ya jumuia ya nchi za kiarabu kutaka mswaada wao wa azimio kuhusu Syria uidhinishwe -Rashia na China zinaendelea kuupinga.Balozi wa Rashia katika Umoja wa mataifa Vitali Tschurkin anasema Umoja wa mataifa haustahiki kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyengine.
"Baraza la Usalama haliwezi kutoa muongozo utaratibu wa siasa ya ndani ya nchi unastahili uwe wa aina gani.Haijatajwa katika muongozo.Hatutaki kuona baraza la usalama likizoweya jambo hilo kwasababu tukianza tu,basi itakuwa shida kuzuwia;hapo litaanza kusema mfalme lazma ajiuzulu,waziri mkuu anabidi ajiuzulu-yote hayo hayalihusu baraza la usalama."
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton amekosoa ile hali kwamba baadhi ya wanachama wa baraza la Usalama wanahofia kitisho cha kutokea hali kama ile ya Libya."Hali hizi mbili hazilinganii "amesisitiza waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani.
Baraza la Usalama linatazamiwa kuendelea na majadiliano yake hii leo kuhusu mswaada uliofanyiwa marekebisho na ambao balozi Tschurkin anautaja kuwa "na baadhi ya mambo yanayotia moyo."
Mwishoni mwa kikao cha jana,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Alain Juppé alisema "kuna uwezekano wa kufikia maridhiano pamoja na Moscow" na hasa kuhusu hatima ya rais Bashar al Assad.
Waziri mwenzake wa Uingereza William Hague amezungumzia "majadiliano pamoja na Rashia na mataifa mengine katika kipindi cha masaa 24 yajayo .
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp/Reuters
Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed