1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama la UN laijadili Mashariki ya Kati

1 Agosti 2024

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya mkutano wa dharura siku ya Jumatano ili kujadili hali ya sasa huko Mashariki ya Kati baada ya mauaji ya maafisa waandamizi wa Hamas na Hezbollah.

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: Loey Felipe/UN Photo/Xinhua/picture alliance

Baraza hilo halikutoa tamko la pamoja ispokuwa kutaja kuwa eneo hilo liko katika hatari ya kushuhudia vita vya kikanda na kuzitaka pande zote kujizuia na kutoa kipaumbele kwa diplomasia.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kwa upande wake kuwa nchi yake itajibu vikali uchokozi wowote kutoka sehemu yoyote huku akisisitiza kuwa Israel itakabiliwa na changamoto kadhaa katika siku zijazo.

Kauli hii ya Netanyahu inajiri baada ya Kiongozi wa Iran Ayatollah Ali Khamenei kuahidi kuwa watalipiza kisasi mauaji ya Kiongozi Mkuu wa Hamas Ismail Hanniyeh ambaye aliuawa nchini Iran hapo jana.

Siku ya Jumanne, wanajeshi wa Israel walisema pia kuwa wamemuua kamanda wa Hezbollah Fouad Shukur katika mji mkuu wa Lebanon Beirut. Ujerumani na Australia zimewataka raia wao kuondoka mara moja nchini Lebanon.

Ulaya, Marekani zataka utulivu kifo cha Haniyeh

Ismail Haniyeh wakati wa uhai wake.Picha: Iran's Presidency/WANA/REUTERS

Umoja wa Ulaya, Marekani na Ujerumani zikitowa wito kwa pande zote kujizuwia na kuifanya hali kuwa mbaya zaidi, huku Iran ikitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kufuatia mauaji ya kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh

Msemaji wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Peter Stano, ameiambia DW kwamba wakati Umoja huo ukiendelea kufuatilia kwa makini mauaji ya Haniyeh, unatowa wito wa kiwango cha juu ya kujizuwia kwa pande zinazohusika na mzozo wa Mashariki ya Kati.

"Umoja wa Ulaya una msimamo wa kimsingi wa kukataa mauaji ya makusudi na kuunga mkono utawala wa sheria, ukiwemo mfumo wa sheria na haki wa kimataifa." Alisema Stano.

Marekani kupitia waziri wake wa mambo ya kigeni, Antony Blinken, imesema haikuhusika na mauaji hayo na wakati huo huo kutoa wito wa kuendeleza mazungumzo ya kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza, ambayo kwa upande wa Hamas yalikuwa yakiongozwa na Haniyeh.

Kiongozi wa Hamas Haniyeh auawa

01:43

This browser does not support the video element.

"Bila shaka nimeona ripoti za mauaji hayo na ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba hakuna kinachopaswa kutuondosha kwenye lengo la kupata makubaliano ya kusitisha mapigano, ambayo ni kwa maslahi ya mateka, wanaotakiwa kurudi nyumbani, kwa maslahi ya Wapalestina wa Gaza wanaoteseka kutokana na haya na kwa maslahi ya kusaka njia bora zaidi sio tu kwa Gaza, bali kwa eneo zima, kwani mambo mengi yanashikana na suala hili." Alisema Blinken.

Soma zaidi: Washirika wa Hamas walaani mauaji ya kiongozi wake

Haniyeh, aliyechukuliwa kama taswira ya diplomasia ya Hamas kwenye uwanja wa kimataifa, aliuliwa pamoja na mlinzi wake akiwa kwenye makaazi rasmi ya maveterani wa vita kaskazini mwa Tehran, majira ya saa nane usiku.

Iran yaapa kulipiza kisasi

Waombolezaji wakiandamana mjini Tehran kulaani mauaji ya Ismail Haniyeh.Picha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Awali, Jeshi la Mapinduzi la Iran lilikuwa limesema kuwa kiongozi huyo angelizikwa mjini Tehran, lakini baadaye chama chake cha Hamas kilisema maiti ya Haniyeh ingelisaliwa na kuagwa mjini Tehran kesho Alkhamis na kisha kwenda kuzikwa nchini Qatar keshokutwa baada ya sala ya Ijumaa.

Wakati mauti yanamkuta, Haniyeh alikuwa kwenye ziara rasmi nchini Iran, ambako alikwenda kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu, Masoud Pezeshkian.

Soma zaidi: Ripoti ya UN yasema Israel inawatesa wafungwa wa Kipalestina

Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, ametuma ujumbe wake kwa Wapalestina, akiwaambia kuwa jukumu la kulipiza kisasi mauaji ya Haniyeh ni la Tehran, ambayo kwenye ardhi yake mauaji hayo yamefanyika.

Hamas tayari imeshasema kwamba italipiza kisasi mauaji ya kiongozi wao huyo mkuu wa kisiasa, ambaye anafahamika kwa kuendesha kampeni ya kimataifa kuwasemea Wapalestina.

Israel, kwa upande wake, imekataa kuzungumzia chochote kuhusu mauaji hayo, lakini msemaji wake, David Mencer, amesema wanajiandaa kwa uwezekano wa mashambulizi ya kulipiza kisasi kutokea Iran.