Baraza la usalama la UN latoa idhini juu ya Libya
20 Machi 2014Azimio hilo lililopitishwa jana Jumatano kwa kauli moja na wanachama wote 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linayaruhusu mataifa wanachama wa Umoja huo kuingia ndani ya meli wanazozishuku kubeba mafuta ghafi, ambazo zimeripotiwa na kamati ya baraza hilo inayofuatilia vikwazo dhidi ya Libya na kuzikagua na kisha kuziamuru kurejesha mafuta hayo nchini Libya.
Azimio hilo limepitishwa baada ya Marekani kuizuia meli iliyokuwa na bendera ya Korea Kaskazini katika pwani ya Cyprus, ambayo waasi wa Libya wamekuwa wakiitumia kusafirisha mafuta nje ya nchi kinyume cha sheria.
Azimio hilo linalaani majaribio yoyote ya kusafirisha nje ya nchi mafuta ghafi kutoka Libya, yanayofanywa kinyume cha sheria. Katika taarifa yake, balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power amewataka wanachama wa umoja huo kulitekeleza azimio hilo haraka, ili kuzuia vitendo vinavyofanywa na watu wanaojaribu kuiba mafuta ya Libya.
Samantha Power amesema utekelezaji wa sheria hizo ni ishara kwa watu wa Libya pamoja na serikali ya nchi hiyo kwamba jumuiya ya kimataifa inaunga mkono uhuru wa Libya na haki yake ya kusimamia rasilimali zake.
Serikali ya Libya na waasi wazozana
Mvutano wa muda mrefu umekuwa ukiendelea kati ya serikali ya Libya na kiongozi wa waasi, Ibrahim Jathran, baada ya kiongozi huyo na wapiganaji wake kuchukua udhibiti wa bandari tatu kubwa za mafuta mwaka uliopita, wakitaka kujitenga kwa eneo la mashariki mwa Libya na kuwa na uhuru zaidi wa kujitawala pamoja na kupata sehemu kubwa ya utajiri wa mafuta. Tangu wakati huo, waasi hao wamekuwa wakijaribu kuuza mafuta.
Serikali ya Libya imewapa waasi hao muda wa wiki mbili kuondoka kwenye bandari hizo au kukabiliwa na mashambulizi ya kijeshi kwa lengo la kumaliza mzozo huo. Kitendo cha waasi hao kudhibiti bandari hizo kubwa za mafuta, kimesitisha uchimbaji wa mafuta kwa mapipa bilioni 1.4 kwa siku na bajeti ya Libya kwa kiasi kikubwa inategemea mapato yatokanayo na mafuta.
Kashfa ya waasi kupakia mafuta ghafi kwenye meli hiyo na kufanikiwa kukikwepa kikosi cha jeshi la majini cha Libya, ilisababisha bunge kumtimua Waziri Mkuu, Ali Zeidan, baada ya kupiga kura ya kutokuwa na imani naye, tarehe 11 ya mwezi huu wa Machi.
Libya bado inapambana kujikwamua kutokana na matatizo yaliyofuatia vuguvugu la mapinduzi ya mwaka 2011, yaliyomuondoa madarakani kiongozi aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Moammar Gaddafi.
Mwandishi: Grace Kabogo/RTRE,AFPE,APE,DPAE
Mhariri: Gakuba, Daniel