1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama lahofia kuongezeka ghasia Kongo

13 Februari 2024

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali makundi yote yenye silaha nchini Kongo na limeelezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa ghasia katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New YorkPicha: Mike Segar/REUTERSS

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika taarifa yake limelaani mashambulizi yaliyoanzishwa mapema mwezi huu na waasi wa M23 karibu na mji wa Goma.

Soma Pia: Jeshi la DRC lapambana na M23 Kivu Kaskazini:

Mapigano yameongezeka hivi karibuni yanayoendeshwa na waasi wa M23 na baadhi ya makundi yenye nguvu yanayomiliki silaha yanayopambana na majeshi ya serikali ya Kongo katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Kulingana na taarifa iliyosomwa na balozi wa Guyana, Carolyn Rodrigues-Birkett, wajumbe wa Baraza la Usalama, waliokutana Jumatatu, 12.02.2024, kulijadili suala hilo, wamelaani makundi yote yenye silaha yanayoendesha vurugu nchini Kongo. Amesema wasiwasi wao mkubwa ni juu ya kuongezeka kwa ghasia na mvutano unaoendelea katika eneo la mashariki mwa Kongo.

Balozi Carolyn Rodrigues-Birkett amesema wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia wamelaani shambulizi la waasi wa M23 la Februari 7 pale ambapo wapiganaji wa M23 waliripotiwa kuuzingira mji wa kimkakati wa Sake siku hiyo kabla ya kuufikia mji wa Goma, ambao ni mji mkuu wa Kivu Kaskazini. Maelfu ya watu walilazimika kukimbia ghasia katika eneo hilo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix TshisekedPicha: Isa Terli /AA/picture alliance

Serikali ya Kongo, Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi zinaituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 ili kukidhi jitihada zake za kulidhibiti eneo hilo lenye rasilimali nyingi za madini, lakini madai hayo yanakanushwa vikali na Rwanda.

Kulingana na waraka wa Umoja wa Mataifa ulioonekana na shirika la Habari la AFP, jeshi la Rwanda linatumia silaha za hali ya juu kama vile makombora kuwasaidia waasi wa M23. Kombora linaloshukiwa kuwa la Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) la kutokea ardhini kwenda angani aina ya (SAM) lilirushwa kuilenga ndege isiyo na rubani ya Umoja wa Mataifa mnamo siku ya Jumatano iliyopita lakini halikufanikiwa kuilenga droni hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Vikosi vya Umoja wa Mataifa vimekuwemo nchini Kongo kwa takriban miaka 25, lakini vinalaumiwa kwa kushindwa kuwalinda raia dhidi ya makundi yenye silaha.

Soma Pia: Raia wa Kongo wafurahia kuondoka wanajeshi wa Afrika Mashariki

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura mwezi Disemba mwaka uliopita na kukubali matakwa ya serikali ya Kongo ya kuwaondoa walinda usalama wa Umoja wa Mataifa licha ya kwamba hali bado tete nchini humo.

Chanzo: AFP

Mhariri:

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW