1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni tamko la kwanza rasmi kutolewa na Baraza

Mohammed Khelef20 Januari 2015

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa karipio rasmi dhidi ya Boko Haram wakati viongozi wa mataifa ya magharibi na kati ya Afrika wakikutana kupanga mkakati wa kulishinda kundi hilo.

Kampeni ya kupigania kuachiliwa huru kwa wasichana waliotekwa na Boko Haram.
Kampeni ya kupigania kuachiliwa huru kwa wasichana waliotekwa na Boko Haram.Picha: AFP/Getty Images/P. U. Ekpei

Katika taarifa iliyotolewa na rais wa baraza hilo na kuthibitishwa na mataifa 15 wanachama wa chombo hicho cha juu kabisa duniani, umeelezwa wasiwasi mkubwa juu ya harakati za Boko Haram ambazo baraza limesema zinahujumu amani na utulivu kwenye eneo zima la magharibi na kati ya Afrika.

Baraza hilo limeitaka Boko Haram kuacha mara moja vitendo vyake hivyo na kuweka silaha chini na pia kuachiwa haraka kwa watu wote iliowakamata wakiwemo wasichana 276 iliowateka mwezi Aprili mwaka jana. Rais wa sasa baraza hilo, Balozi Cristian Barros Melet wa Chile, alisema kinachofanywa na Boko Haram ni uhalifu wa kivita.

"Baraza la Usalama linatambua kwamba baadhi ya matendo ya Boko Haram yanalingana na uhalifu dhidi ya ubinaadamu na linasisitiza kwamba wale wanaohusika na uvunjwaji wa haki za binaadamu na sheria zinazolinda ubinaadamu wachukuliwe hatua," alisema Balozi Melet.

Kauli ya kwanza rasmi ya Baraza la Usalama

Kauli hiyo ilitayarishwa na Nigeria, ambayo awali ilikuwa ikisita kulitaka Baraza hilo kulijadili suala la Boko Haram, licha ya kuwa mwanachama wa Baraza la Usalama. Mara ya mwisho baraza hilo ilipotoa kauli juu ya Boko Haram, ilikuwa ni mwezi Aprili mwaka jana, wakati kundi hilo lilipowateka wasichana 276 wa skuli moja kijijini Chibok.

Kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau.Picha: picture alliance/AP Photo

Hata hivyo, kauli yake hiyo ilikuwa ni taarifa tu kwa vyombo vya habari, ambayo haikuwa sehemu ya rikodi rasmi za baraza hilo. Kauli ya jana inaitwa kauli ya rais, ambayo inakuwa sehemu ya rikodi rasmi na pia ni ya pili kwa umuhimu baada ya azimio rasmi la baraza hilo.

Kauli hii inakuja huku mataifa ya eneo la kati na magharibi mwa Afrika yakikutana mjini Niamey, Niger, kujadiliana hatua za kuchukua dhidi ya kitisho cha Boko Haram, zikiwemo hatua za kijeshi.

Baraza la Usalama limezitolea wito nchi hizo kuunda kikosi cha pamoja cha dharura kuikabili Boko Haram katika operesheni ambayo itakuwa endelevu na yenye ufanisi.

Ijumaa iliyopita, bunge la Chad lilipiga kura ya kuidhinisha jeshi lake kuingia Nigeria na Cameroon kuwasaidia wanajeshi wa huko kwenye vita vyao dhidi ya Boko Haram, na hapo jana wanajeshi hao wakaanza rasmi operesheni yao.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga