Baraza la Usalama lakutana kuhusu mzozo wa Palestina
5 Januari 2023Balozi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, Riyadh Mansour, alizungumza kwenye mkutano maalum na mabalozi wa nchi za Kiarabu, wawakilishi wa mataifa 57 wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, na wajumbe 120 wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote.
Baadaye, akisindikizwa na mabalozi wengine 20 wanaowakilisha nchi zao kwenye Umoja wa Mataifa, Mansour alisema mkutano wa siku ya Alhamisi (Januari 5) wa Baraza la Usalama unaoungwa mkono pia na Umoja wa Falme za Kiarabu, China, Ufaransa na Malta lazima usimame dhidi ya kile alichokiita "mazingira ya uharibifu" yanayojengwa na serikali mpya ya muungano wa vyama vya siasa kali nchini Israel.
"Mashambulizi haya sio tu ni dhidi ya maeneo yetu matakatifu ya Msikiti wa Al-Aqsa na Haram A-Sharif, bali pia yanafanyika kwa sababu ya serikali hii yenye siasa kali kabisa ya Israel inaongeza uchokozi wa ziada dhidi ya maeneo yetu ya Kikristo, makaburi ya Wakristo, unaofanywa na walowezi wenye siasa kali. Haya ni mazingira ya uharibifu. Lazima jumuiya ya kimataifa ipinge kwa kauli moja." Alisema balozi huyo.
Ukosoaji waongezeka
Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Siasa na Ujenzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa, Khaled Khiare, atatowa taarifa fupi mbele ya Baraza la Usalama, kwa mujibu wa msemaji wa Umoja huo, Stephane Dujarric.
Balozi wa Jordan kwenye Umoja wa Mataifa, Mahmoud Hmoud, alisema nchi yake ambayo mfalme wake Abdullah wa Pili ndiye mwangalizi wa maeneo matakatifu kwa Waislamu na Wakristo, "imetiwa hofu sana na uingiliaji wa Ben-Gvir na serikali ya Israel."
"Hiki ni kitendo cha siasa kali kinacholenga kurejesha machafuko yasiyokwisha. Baraza la Usalama linapaswa kubeba jukumu lake kwa umakini na kusimamisha majaribio kama haya." Alisema balozi huyo.
Ziara ya siku ya Jumanne (Januari 3) ya waziri mpya wa Usalama wa Taifa,Itamar Ben-Gvir, kwenye eneo takatifu linalojuilikana na Mayahudi kama Hekalu la Mlimani na kwa Waislamu kama Haram al-Sharif, ilizuwa ukosoaji mkubwa kutoka ulimwengu wa Kiislamu, kauli ya upinzani kutoka Marekani, na kuongeza wasiwasi wa machafuko baada ya makundi ya wanamgambo wa Kipalestina kutishia kuchukua hatua kali.