Walinda usalama wa UN wakabiliwa na vitisho
25 Mei 2021Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumatatu lilitoa tamko la kulaani vikali vitendo vya hujuma ya kushambuliwa na kuuwawa wanajeshi wa Umoja huo na kusisitiza juu ya umuhimu mkubwa wa usalama wa wanajeshi wake zaidi ya 90,000 walioko kwenye ujumbe wa kulinda amani katika katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,Sudan Kusini na Mali hadi mashariki ya Kati India na Pakistan.
Baraza hilo la usalama limesema katibu mkuu Antonio Guterres na nchi zinazochangia wanajeshi na askari katika operesheni za kulinda amani wanapaswa kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha kwamba walinda amani wana raslimali za kutosha,vifaa na silaha pamoja na kuwa na mafunzo ya kuweza kukabiliana na vitisho ikiwemo kitisho cha mabomu ya kutegwa ardhini,vifaa vingine vya miripuko katika maeneo ya vita na vifaa vya miripuko ya kutengenezwa kwa mikono.
Tamko hilo liliandaliwa na rais wa China na liliidhinishwa na nchi zote 15 wanachama wa baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa katika mkutano wa wazi ambapo mkuu wa shughuli za kulinda amani za Umoja huo wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix alisema wanajeshi wanaofanya kazi kwenye ujumbe wa kulinda amani wanafanya kazi katika mazingira magumu ambako wanakabiliwa na ongezeko kubwa la mashambulizi yanayofanywa na wanaochukia wanajeshi hao. kwa mujibu wa Lacroix wanajeshi 15 wa kulinda amani wameshapoteza maisha yao kutokana na vitendo vilivyokusudiwa vya kuwashambulia.
Aidha ameongeza kusema kwamba juu ya kuwepo mazingira ya kutokubalika na mashambulizi ya moja kwa moja,masuala yanayohusiana na usalama wa walinda amani kama vile ajali za magari na maradhi pia ni mambo mengine yanayosababisha vifo na yanaweza kuathiri kwa kiwango kikubwa uwezo wa walinda amani katika utekelezaji wa majikumu yao. Lakini pia mkuu huyo wa shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa amezungumzia juu ya umuhimu wa bajeti ya kusimamia harakati hizo za kulinda amani.
" Kuepusha hatua zisizohitajika za kupunguza bajeti ya makao makuu na shughuli za kijeshi kutatusaidia sisi kuhakikisha juhudi za kuimarisha usalama wa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa zinaendelea. Bila shaka tumejitolea kusimamia na kutumia kwa uangalifu fedha zinazotolewa na nchi wanachama,lakini wakati huohuo nafikiri sote tunaelewa kwamba kulinda amani kunahitaji raslimali nyingi na hasa katika wakati huu wa mazingira ya changamoto na hatari''
Katika mwaka 2020 Lacroix ametowa mfano kwamba wanajeshi 13 walikufa kutokana na matukio ya kushambuliwa lakini 15 walikufa kutokana na ajali na 81 walikufa kutokana na maradhi,ingawa pia alisema hali hiyo imechangiwa na janga la Covid-19.Lacroix amesema teknolojia imeimarisha uwezo wa walinda amani na hatua ya kujiweka tayari,kutokana na kuwepo teknolojia kama mifumo ya kutoa onyo la mapema na ndege zisizokuwa na rubani. Lakini pia amegusia kwamba Umoja wa Mataifa umepiga hatua katika kuziunga mkono nchi ambazo zina vikosi vya kulinda amani katika juhudi zao za kuwafikisha mbele ya sheria wanaohusika na vitendo vya uhalifu dhidi ya walinda amani,ikitolewa mfano wa watu 6 walishtakiwa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati mwanzoni mwa mwaka 2020 na Marchi 2021.