1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Baraza la Usalama lapitisha azimio la usitishaji vita Gaza

Sylvia Mwehozi
25 Machi 2024

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kutaka usitishaji mara moja wa mapigano baina ya Israel na wanamgambo wa Hamas na kuachiliwa mara moja kwa mateka wote waliosalia.

Marekani| New York | Baraza la Usalama
Sehemu ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: Craig Ruttle/AP Photo/picture alliance

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kutaka usitishaji mara moja wa mapigano baina ya Israel na wanamgambo wa Hamas na kuachiliwa mara moja kwa mateka wote waliosalia bila masharti baada ya Marekani kujizuia leo kupiga kura.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza siku ya Jumatatu limetaka kusitishwa kwa mapigano huko Gaza, huku Marekani, mshirika wa Israel ambayo ilipiga kura ya turufu katika azimio lililopita, ikijizuia mara hii kupiga kura.

Mtoto wa Kipalestina akisubiri kupokea chakula wakati wa RamadhanPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Azimio hilo, ambalo linataka "kusitishwa mara moja kwa mapigano" wakati wa mwezi mtukufu wa Kiislamu unaoendelea wa Ramadhani na kupisha njia kwa mapatano "ya kudumu", limepitishwa hii leo huku wajumbe 14 wa Baraza la Usalama wakipiga kura ya ndio. Azimio hilo lililikuwa limependekezwa na wanachama 10 wa kuchaguliwa wa Baraza la Usalama.

Soma: Baraza la Usalama lashindwa kupitisha azimio la kusitisha vita Gaza

Azimio hilo la Baraza la Usalama pia "linasisitiza haja ya udharura wa kupanua usambazaji wa misaada ya kibinadamu na kuimarisha ulinzi wa raia katika Ukanda wote wa Gaza na linasisitiza mahitaji ya kuondolewa vikwazo vyote kwa utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa kiwango kikubwa."

Redio ya jeshi la Israel imeripoti muda mfupi kabla ya mkutano wa baraza kuanza kwamba Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ataghairi ujumbe uliopangwa kwenda Washington ikiwa Marekani haitapiga kura ya turufu dhidi ya azimio hilo.

Marekani: Israel imruhusu Mkuu wa UNRWA kutembelea Gaza

Hospitali katika Ukanda wa Gaza zaelemewa

02:03

This browser does not support the video element.

Marekani mara kwa mara imezuia maazimio ya kusitisha vita wakati ikijaribu kutafuta uwiano baina ya kuiunga mkono Israel na misaada ya kijeshi na upande mwingine kuelezea kufadhaika kwake na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wakati idadi ya vifo vya raia katika ukanda wa Gaza ikiongezeka.  Israel imelikosoa Baraza la Usalama kwa maazimio yaliyopita ambayo hayakulaani Hamas.

Soma pia: Urusi na China zapinga rasimu ya azimio lililopendekezwa na Marekani la usitishaji mapigano Gaza

Hayo yakijiri Israel imesema kuwa itaacha kufanya kazi na shirika la misaada la Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Gaza UNRWA, ikilishutumu shirika hilo kuendeleza migogoro. Msemaji wa serikali ya Israel David Mencer amewaeleza waandishi wa habari hii leo kwamba shirika la "UNRWA limekuwa sehemu ya matatizo" na wataacha kufanya kazi nalo. Ameongeza kuwa wanaondoa kabisa shughuli za UNRWA kwasababu inaendeleza mizozo badala ya kujaribu kupunguza mizozo.

Wapalestina wakiomboleza mwili wa mfanyakazi mwenzao wa Umoja wa Mataifa aliyeuawa katika shambulizi la anga la IsraelPicha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Wakati Israel ikitoa angalizo hilo, shirika lenyewe la UNRWA limesema kwamba hakuna misaada ya kiutu inayoingia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza licha ya tahadhari zilizotolewa kuhusu kitisho cha njaa. Taarifa hiyo inafuatia kauli iliyotolewa Jumapili na mkuu wa shirika hilo iliyosema mamlaka za Israel ziliarifu kwamba hazitotoa kibali chochote cha msafara wa shirika hilo wa chakula kuingia kaskazini mwa Gaza, ambako Philippe Lazzarini anasema watu wako kwenye ukingo wa baa la njaa.

UN: Ni hatari kusitisha ufadhili kwa shirika la UNRWA

Lazzarini ameongeza kuwa hatua ya kuzuia misaada ya UNRWA kuingia kaskazini mwa Gaza ni "jambo la kuchukiza na la kimakusudi katika kuzuia usaidizi wa kuokoa maisha uliotokana na baa la njaa lililotokana na binadamu. Israel mara kwa mara imekataa shutuma za kuzuia usambazaji wa misaada na badala yake inalishutumu shirika hilo kwa kutosambaza misaada inavyotakiwa.