Baraza la Usalama lashindwa kupitisha azimio kuhusu Gaza
22 Machi 2024Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limeshindwa kupitishaazimio la kutaka kusitishwa mara moja kwa vita katika ukanda wa Gaza kama sehemu ya makubaliano ya kubadilishana mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina, baada ya China na Urusi kupinga azimio hilo lililowasilishwa na Marekani.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield, ameliambia Baraza hilo kwamba mataifa mengi yalipiga kura kuunga mkono azimio hilo lakini kwa bahati mbaya, Urusi na China ziliamua kupinga.
Thomas Greenfield ameendelea kusema kuwa "azimio la baraza la usalama halina maana kubwa ikiwa halitatekelezwa. Hii ndio maana Marekani, Misri na Qatar zinashughulika katika kanda hiyo kuhakikisha kusitishwa mara moja kwa mapigano kama sehemu ya kuachiwa huru kwa mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas na makundi mengine hali itakayowezesha kushughulikia mzozo mbaya wa kibinadamu katika ukanda wa Gaza."
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia, kabla ya kupigwa kura aliwataka wanachama wa baraza la usalama kutoliunga mkono Azimio la Marekani akisema limetengenezwa kwa kiasi kikubwa kwa misingi ya kisiasa.