1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mike Johnson Spika mpya wa Baraza la Wawakilishi la Marekani

Angela Mdungu
26 Oktoba 2023

Hatimaye baraza la wawakilishi la Marekani limemchagua Mike Johnson kuwa spika mpya. Hatua hiyo imehitimisha wiki kadhaa za mkwamo katika baraza la hilo wakati kukiwa na mizozo ya ndani na nje ya Washington.

Spika wa bunge la wawakilishi la Marekani Mike Johnson
Spika wa bunge la wawakilishi la Marekani Mike JohnsonPicha: ALEX WONG/Getty Images/AFP

Mike Johnson ambaye ni mshirika asiyefahamika sana wa aliyekuwa Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ameungwa mkono kwa kauli moja na chama chake kuongoza baraza la wawakilishi ambalo lilisimamisha shughuli zake tangu Kevin McCarthy alipong'olewa kwenye kiti chake Oktoba 3.

Mara baada ya hotuba yake, spika huyo mpya aliwasilisha azimio la kuiunga mkono Israel ambayo ni mshirika wake mkubwa katika mashariki ya kati kwenye vita vyake dhidi ya kundi la Hamas. Azimio hilo lilipita kwa kuungwa mkono na walio wengi.

Soma zaidi: Mgawanyiko wa ndani wa Republican umelifanya Baraza hilo kutoweza kuzungumzia vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati wala Ukraine

Kufuatia kuteuliwa kwake, Rais Joe Biden alimpigia simu na kumpongeza spika huyo na kusema kuwa ni wakati wa kila mmoja kufanya kazi kwa kuwajibika wakati kukiwa na changamoto za kuipa fedha serikali na kuzisaidia nchi za Ukraine na Israel.

Changamoto lukuki zitamkabili spika mpya

Mike Johnson anatarajiwa kukabilliana na uwezekano wa serikali kuvunjika suala ambalo linaweza kutishia kibarua chake, isipokuwa tu kama atafanikiwa kupunguza bajeti ya mwaka 2024 na kuwashughulikia mahasimu wake kama vile kiongozi wa  walio wengi katika bunge la seneti Chuck Schumer na rais Anatarajiwa pia kukiongoza na kuliunganisha baraza la wawakilishi lenye mgawanyiko mkubwa katika mivutano ijayo kuhusu kuzifadhili Israel na Ukraine zilizo kwenye vita.

Mike Johnson akipongezwa na aliyekuwa spika wa baraza la wawakilishi la Marekani Kevin McCarthyPicha: ALEX WONG/Getty Images/AFP

Johnson, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kutokea jimbo la Louisiana, ameshinda kiti hicho baada ya kuwa mgombea wa nne ndani ya mwezi huu kuteuliwa kuwania kiti cha uspika, ambacho kimekuwa wazi tangu Kevin McCarthy alipopinduliwa na wajumbe wa chama chake walioasi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW