1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barcelona mabingwa wa La Liga 2019

Sylvia Mwehozi
28 Aprili 2019

Klabu ya Barcelona imenyakua ubingwa wake wa 8 wa ligi kuu ya Hispania La liga katika kipindi cha miaka 11 baada ya kuifunga Levante bao 1-0 kwenye mchezo Jumamosi.

Spanien Fußball FC Barcelona - UD Levante
Picha: Getty Images/D. Ramos

Lionel Messi aliyetokea benchi katika kipindi cha pili alipachika bao la ushindi dakika ya 62 na kuifanya klabu hiyo kuwa bingwa mara 26 katika historia ya la liga, ikiwa ni ya pili nyuma ya Real Madrid iliyonyakua ubingwa huo mara 33.

Golikipa wa Levante alifanikiwa kulilinda lango lake katika kipindi cha kwanza na kuokoa mikwaju kutoka kwa Luiz Suarez na Philippe Coutinho. Messi amekabidhiwa kikombe na rais wa shirikisho la kandanda la Hispania Luis Rubiales na kufuatiwa na shamra shamra uwanjani.

Messi alikuwa amepumzika kwa kipindi chote, aliingia baadae akiwa amepachika kimiani magoli 11 katika jumla ya michezo 9 katika uwanja wa nyumbani wa Camp Nou dhidi ya Levante. Kocha wa Barcelona Ernesto Valverde atakuwa na kibarua kingine katikati mwa wiki cha nusu fainali ya michuano ya klabu bingwa Ulaya, atakapovaana na Liverpool.

Soma Zaidi...

Valverde amewasifu wachezaji wake kwa mafanikio hayo akisema, "ligi ni shughuli ya kila siku. Kulikuwa na wiki ambayo tulipoteza dhidi ya Leganes. Lakini wakati timu inaposimama nyakati ngumu, inasimama haswa". Alipoulizwa mchango wa Messi katika klabu hiyo, alitania  akisema ni "kidogo sana" kabla ya kuongeza kuwa "Messi ni mchezaji anayeleta utofauti. Siku zote kuna mchezaji ambaye ni zaidi ya wengine na hakika ni yeye."

Lionel Messi akishangilia goli dhidi ya Levante Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Fernandez

Hii ni ligi ya pili kwa kocha Velverde katika kipindi cha miaka miwili na ameongeza kuwa "jambo gumu sio kushinda, bali ni kuendelea kushinda na kuwa na kiu ya kushinda tena."

Ushindi wa Barca unaipatia pointi 9 mbele ya Atletico Madrid iliyo nafasi ya pili ikiwa imebakisha michezo mitatu na pia inakimbizana na Madrid kuwania nafasi ya pili. Atletico waliibamiza Valladolid bao 1-0 na kuilazimu Barcelona kuhitaji ushindi ili kuhitimisha mbio za ubingwa kabla ya kusonga mbele na michuano ya klabu bingwa Ulaya. 

ap/dpa

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW