Barcelona yaishinda Sevilla katika fainali ya UEFA Super Cup
12 Agosti 2015Washindi wa kombe la Europa Sevilla waliwashangaza Bacelona ambao ni washindi wa klabu bingwa barani Ulaya – Champions League, baada ya Ever Banega kufunga goli la kwanza kupitia freekick yenye ufundi mkubwa.
Mshambuliaji nyota Lionel Messi alifunga mara mbili kupitia mikwaju ya adhabu na kuifanya Barca kuongoza kwa goli 2-1 kabla ya Rafinha na Luis Suarez kutikisa nyavu za Sevilla na kufanya mambo kuwa 4-1.
Kisha Sevilla wakaanza kupambana kuyarejesha magoli hayo ambapo Jose Antonio Reyes, Kevin Gameiro na Yevhen Konoplyanka walifunga kila mmoja na kuulazimisha mpambano huo kwenda dakika 30 za nyongeza kabla ya Pedro kuifungia Barca goli la ushindi katika kipindi cha pili cha muda wa ziada.
Hayo ni mafanikio makubwa kwa Barca tokea mwaka 2011 baada ya kushinda mataji matano mfululizo na kuifikia AC Milan ya Italia yenye rekodi sawa na hiyo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo