1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barcelona yatwaa ubingwa wa ligi kuu ya Uhispania

19 Mei 2015

FC Barcelona imenyakua taji lake la tano katika misimu saba ya Ligi ya Uhispania La Liga baada ya bao safi la Lionel Messi kuipa ushindi timu hiyo dhidi ya Atletico Madrid

Spanien Fußballer FC Barcelona sind spanischer Meister 2015
Picha: Reuters/J. Medina

Real Madrid hata hivyo imepata ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Espanyol Barcelona lakini Barca haiwezekani tena kukamatwa ikiwa na pointi nne zaidi ya Real ikiwa bado mchezo mmoja.

Kocha wa Barcelona Luis Enrique anaamini kwamba taji la 23 la klabu yake katika La Liga linaweza kuwa fursa ya kushuhudia kipindi kirefu cha mafanikio na uwezekano wa kunyakua mataji matatu msimu huu.

Barca inakwaana na Athletic Bilbao nyumbani katika kombe la Mfalme Copa del Rey hapo Mei 30 kabla ya kuikabili Juventus Turin katika fainali ya Champions League tarehe 6 Juni.

Luis Enrique aliombwa huduma yake na kuandikishwa pamoja na wachezaji saba wapya majira ya joto mwaka jana baada ya kampeni ya kwanza bila taji lolote katika muda wa miaka sita na kusifu jinsi wachezaji hao walivyojibu katika kile alichoeleza kuwa ni msimu wa mpito.

Barcelona sasa inalenga mataji mengine mawili yaliyosalia msimu huu; Champions League na Copa Del ReyPicha: Reuters/A. Comas

"Ni matumaini yangu kuwa ni enzi mpya. Tunapaswa kuonesha kwamba tunastahili kushinda vikombe. Tuna fainali mbili mbele yetu na tunapaswa kuonesha kuwa tuna uwezo kuliko wapinzani wetu, " amesema.

Kwa upande wa mahasimu wao wakubwa Real Madrid , kama kuna funzo kubwa alilopata kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti ni kugundua katika misimu yake miwili nchini Uhispania kwamba kubweteka si jambo zuri katika klabu hiyo tajiri kabisa duniani kwa mapato. Baada ya kuiongoza Real Madrid kupata taji lake la kumi , La Desima msimu uliopita na ubingwa wa kombe la Mfalme, Real imeshindwa kupata ubingwa wowote msimu huu na kuzusha fununu juu ya majaaliwa ya kocha huyo raia wa Italia.

Mkurugenzi wa klabu hiyo Emilio Butragueno amekataa kuthibitisha kwamba Ancelotti atatumikia mkataba wake hadi mwisho, mkataba ambao unamalizika baada ya msimu ujao, baada ya Real kuondolewa katika kinyang'anyiro cha Champions League Jumatano iliyopita. na uventus Turin.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Uhispania na timu ya Real amefanya hivyo tena kufuatia ushindi wa Barcelona dhidi ya Atletico Madrid jana Jumapili, ushindi ulioihakikishia Barca ubingwa wa La Liga.

Miongoni mwa majina yanayohusishwa na kazi hiyo ya Ancelotti ni pamoja na kocha wa Borussia Dortmund Juergen Klopp ambaye anaiacha klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu, pamoja na Jose Mourinho, Rafa benitez na Julen Lopetegui.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe 7 dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga