1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barnier: Mazungumzo ya Brexit yanaelekea pazuri

Sylvia Mwehozi
17 Desemba 2020

Mjumbe mkuu wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya Brexit Michel Barnier amesema mazungumzo ya kibiashara na Uingereza yanaendelea vizuri, yakinuia kuupatia ufumbuzi mkwamo huo katika kipindi cha wiki mbili zijazo,

UK Michel Barnier
Picha: Peter Nicholls/REUTERS

Kiongozi huyo wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya BrexitMichel Barnier ameandika katika ukurasa wa Twitter kwamba, "maendeleo ni mazuri, lakini bado vikwazo vimesalia". Barnier ameendelea kusema kuwa watatia saini mkataba pekee utakaolinda maslahi na kanuni za Umoja wa Ulaya.

Pauni ya Uingereza imeimarika dhidi ya Dola ya Kimarekani baada ya waziri wa mambo ya ndani Priti Patel kusema kwamba mazungumzo yameingia katika "handaki", msemo wa Umoja wa Ulaya unaomaanisha hatua za mwisho. Waziri Mkuu wa Uingereza Borris Johnson, atakuwa na kibarua cha kuamua ikiwa akubaliane na mkataba hafifu kutoka Umoja wa Ulaya ama kuhatarisha vurugu za kiuchumi na kisiasa zitokanazo na sakata hilo.

Afisa mmoja wa Umoja wa Ulaya ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema tofauti katika masuala ya uvuvi bado hazijapatiwa ufumbuzi, na kwamba hata mambo mengine madogo bado yanahitaji kupigwa msasa. Lakini afisa mwingine kutoka upande wa Uingereza ambaye naye hakutaka kutajwa majina yake, ameeleza kwamba "pande zote mbili bado zinatofautiana kwenye masuala muhimu".

Borris Johnson na Ursula von der LeyenPicha: Olivier Hoslet/AFP

Hapo Jumatano, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alisema kwa hivi sasa "kuna njia nyembamba" kuelekea makubaliano, ingawa mafanikio siyo ya uhakika. Michael Gove, ambaye ni mratibu wa Brexit katika serikali ya Johnson, anasema wajumbe walikuwa wakifanya kazi kwa bidii, lakini makubaliano yoyote yatapaswa kuheshimu uhuru wa Uingereza.

''Ni kweli kwamba serikali ya Uingereza imekuwa wazi juu ya umuhimu wa kudumisha uhuru, haki ya kutengana na udhibiti kamili wa maji yetu. Hatutakuwa na utata juu ya hilo lakini tunadhamira ya kuweza kufikia makubaliano ya biashara huru na wajumbe wetu wanafanya kazi kwa bidii kufikia lengo hilo,'' alisema Gove.

Masuala mawili muhimu ambayo bado ni kizungumkuti katika mazungumzo hayo ni kiwango cha ushindani sawa na haki za uvuvi. Waziri Mkuu Johnson anauchukulia mchakato wa Brexit kama fursa ya kuijenga Uingereza kuwa taifa thabiti kiuchumi ambalo litakuwa imara zaidi ya washindani wake na hivyo hataki kuendelea kuwepo katika kivuli cha Umoja wa Ulaya na sheria zake kwa miaka mingi ijayo.

Uingereza ilijiunga na umoja huo mwaka 1973 na kujiondoa rasmi Januari 31, na tangu wakati huo imekuwa chini ya kipindi cha mpito ambacho kanuni za biashara na usafiri hazijabadilika.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW