1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barroso alihutubia bunge la Ulaya kuhusu hali ya Umoja wa Ulaya

Josephat Nyiro Charo7 Septemba 2010

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barosso, kwa mara ya kwanza amelihutubia bunge la Ulaya kuhusu hali halisi ya umoja huo mjini Strasbourg

Jose Manuel Barroso akilihutubia bunge la Ulaya, StrasbourgPicha: AP

Katika hotuba hiyo ambayo huenda ikamuweka katika hali ngumu ya kukabiliwa na upinzani kutoka kwa nchi 27 za Umoja wa Ulaya, Barroso ameutaka umoja huo uainishe uwezo wake mkubwa wa kiuchumi na misuli yake ya kidiplomasia. Katika tukio linanuia kuiga hotuba ya mwaka inayotolewa na marais wa Marekani katika bunge la nchi hiyo, Barroso, ameeleza matumaini yake kuhusu uchumi wa Ulaya lakini akahimiza kuimarishwa kwa soko la pamoja ili kuinua zaidi uchumi na kutengeneza ajira mpya.

Barroso ameshangiliwa na wabunge wakati wa hotuba yake ya asubuhi ya leo iliyodumu dakika 30, pale alipozungumzia kufukuzwa kwa watu wa jamii ya Roma au Gypsies, kutoka nchini Ufaransa.

"Kila mtu barani Ulaya sharti aheshimu sheria na serikali lazima ziheshimu haki za binadamu, zikiwemo haki za jamii za wachache. Ubaguzi na chuki dhidi ya wageni havina nafasi barani Ulaya."

Hata hivyo Martin Shulz, mwenyekiti wa kambi ya Wasoshalisti katika bunge la Ulaya amesema Barroso ameonyesha udhaifu miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, na hata kuhusu hatua ya Ufaransa kuwafukuza Waroma. Amemkosoa Barroso kwa kushindwa kuilaani Ufaransa kwa mpango wake wenye utata wa kuwafukuza wahamiaji wa jamii ya Waroma na kuwarejeshe makwao huko nchini Romania na Bulgaria.

Hotuba ya Barroso imekita zaidi kwenye juhudi za kuimarisha uchumi wa Umoja wa Ulaya, akisisitiza zaidi masuala ya ajira, utafiti na uvumbuzi.

"Huu ni wakati wa muhimu kwa Ulaya. Umoja wa Ulaya lazima uonyeshe kuwa ni zaidi ya maamuzi ya serikali 27 za nchi wanachama. Ama tunaogelea pamoja au tuzame maji kila mmoja kivyake. Tutafaulu tu kama wakati tunaposhirikiana tutafikiria kama Ulaya."

Barroso amesema uchumi wa Ulaya ni imara zaidi kuliko mwaka mmoja uliopita na kuzipongeza juhudi za nchi wanachama. Hata hivyo ameonya kuwa sio nchi zote wanachama zinazoshiriki katika juhudi za kuufufua uchumi. Amesema kasi ya ukuaji wa kiuchumi inaongezeka, ingawa sio sawa katika nchi zote wanachama na kuongeza kuwa uchumi unatarajiwa kukua zaidi kuliko ilivyokadiriwa hapo awali.

Kinyume na hotuba za marais wa Marekani katika bunge lao ambazo hufuatiliwa na mamilioni ya Wamarekani, wasikilizaji wa hotuba ya Barroso walikuwa wabunge wa Ulaya. Na kutokana na wasiwasi kwamba Barroso angezungumza peke yaje bungeni, wabunge walitishwa na wakuu wao kwamba wangetozwa faini kama hawangekwenda bungeni kuisikiliza hotuba ya kiongozi huyo.

Kinyume na hotuba za Marekani, wabunge wa Ulaya wamepewa fursa ya kutoa hisia zao kuhusu hotuba ya Barroso.

Mwandishi: Hasselbach, Christoph (DW Brüssel)/ Josephat Charo

Mhariri:Abdul-Rahman