1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barua kutoka Dar: Hatua za lala salama kuelekea uchaguzi

Anaclet Rwegayura15 Oktoba 2020

Kampeni za uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani nchini Tanzania zinakaribia mwisho, lakini watu kwa ujumla wanaamini kuwa bado wanajifunza kuhusu utawala wa kidemokrasia na jinsi kampeni zinaweza kuboreshwa siku zijazo.

Tansania Dar Es Salaam Kigamboni Brücke Eröffnung
Picha: Imago/Xinhua

Kila uchaguzi umekuwa mchakato wa kujifunza kwa viongozi na kwa wapiga kura. Tofauti na nchi nyingine ambako uchaguzi unakuwa sababu ya mizozo, mazingira ya Tanzania yanaendelea kutia moyo ingawa yametawaliwa na chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho huweka mwelekeo kwa sababu wapinzani wake ni dhaifu.

Ijapokuwa vyama vya upinzani vimekuwepo kwa karibu miongo mitatu, vinashindwa kupenya ukuta wa umaarufu wa CCM. Vimekuwa vikishinda viti kadhaa vya ubunge na serikali za mitaa lakini CCM inavishinda kutokana na rekodi yake ya utendaji kwa kuonyesha kile inachofanya. Hii ndio inaleta tofauti kubwa.

Njia ya chama hicho iko kwenye mwendelezo badala ya kuanza upya. Wapinzani wake huahidi tu kwa watu wakati wa uchaguzi na kuishia hapo. Havioneshi utambuzi wa matatizo na kuweka mkakati wa kupata suluhisho ambazo zinaweza kufanya sera zao ziwe muhimu kwa watu.

Mgombea urais kupitia Chadema Tundu LissuPicha: AFP

Masuala mengi ni muhimu katika mbio hizi za uchaguzi kuanzia suala la usawa na kuheshimiana katika siasa za vyama vingi na kuzingatia yale ambayo wapiga kura wanataja kama vipaumbele vya maendeleo ya kitaifa. Kwa CCM kipaumbele ni kudumisha ukuaji wa uchumi, maisha bora ya wananchi na kulinda umoja wa taifa. Kila kura katika haya ni muhimu sana.

Ukuaji wa uchumi na maendeleo ni mada ya siku zote nchini Tanzania. Wagombea wanaowania uchaguzi mwaka huu wanatoa tafsiri tofauti za kile wanachokiona kama maisha bora kwa watu na maendeleo kwa taifa.

Hakuna hata mmoja wa wagombea hawa anaweza kuelezewa kama kiumbe tofauti wa kisiasa kutokana na kile wanachosema katika misafara ya kampeni. Wote wana masilahi ya kitaifa moyomi lakini ilani za vyama vyao zina njia tofauti za kutimiza malengo hayo.

Wanaweza kutokubaliana juu ya mambo machache, lakini sio juu ya umuhimu wa amani ya kitaifa, utawala wa sheria na amani, umiliki wa maliasili na usawa wa raia.

Sasa tunapotazamia kuvinjari mawimbi ya mwishoni kufikia uchaguzi mkuu na kupata uongozi mpya au tuseme ulioboreshwa kwa miaka mitano ijayo, watu wengine wanasema kuwa hoja za kufunga kampeni hazitabadilisha chochote.

Kwa mchango wa vyombo vya habari tangu mwanzo wa kipindi cha kampeni, wanasema ujumbe muhimu wa wagombea umewafikia wapiga kura. Hii inahusu zaidi wagombea urais wa Muungano kwa Chama Cha Mapinduzi, Chadema na CUF.

Wafuasi wa chama tawala CCM wakati wa kampeni Picha: DW/E. Boniphace

Mikutano yao imevutia umati katika miji kadhaa. Umuhimu wao, hata hivyo, utadhihirika kutokana na jinsi wapiga kura wataonesha mgombea wa chaguo lao. Ni kawaida katika mbio ngumu kama hizi washiriki wengine huachwa njiani.

Kwa hiyo, uchaguzi utakuwa kwa wale wanaohitimisha mbio wakidhihirisha kuwa ni washindani kweli wa kuchaguliwa. Mpaka sasa hakuna mgombea aliyejiondoa rasmi kwenye kinyang'anyiro lakini baadhi yao wameshindwa kuendelea na mdundo wake.

Kutafuta kura kunapaswa, katika siku zilizobaki, kuwapa nafasi ya kutafakari wale ambao hawajaamua ni nani wampigie kura.. Licha ya hali isiyo ya uhakika kutokana  na janga la maradhi ya Korona, Watanzania hapana budi watulie ili wafanye uchaguzi sahihi.

Kuwa mbunge nchini Tanzania imekuwa njia moja ya kustaafu vizuri hasa kwa wafanyikazi wa umma ambao hawana kipato cha kutegema baada ya kustaafu. Baada ya utumishi wa miaka mingi, wanastahili kustaafu wakiwa na amani, sio ukata.

Wapiga kura wa Tanzania wachague viongozi na wabunge wanaotambua mabadiliko ya sasa katika maisha ya kazi na changamoto za kila siku za watu wasio na kazi.

Watu wana hamu ya kuona uongozi ujao ukifanya kazi kwa njia mpya za kuharakisha maendeleo kwa kuzidisha  tija na ufanisi. Uovu mmoja ambao unasumbua akili zetu zaidi ni ufisadi ambao unabaki kupiga chenga katika jamii.