1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barua kutoka Dar: Tatizo la utoro wa wanafunzi Tanzania

Anaclet Rwegayura2 Februari 2023

Wanafunzi wa msingi na sekondari wanatakiwa kuwa shuleni baada ya mwaka wa masomo kufunguliwa lakini wengine hawajaripoti shuleni kama anavyoandika Anaclet Rwegayura katika barua kutoka Dar akitizama utoro wa wanafunzi.

Videostill AOM Africa on the Move Tansania Schule für Kinder mit Behinderung
Picha: DW/M. Grundlach

Na Anaclet Rwegayura

Suala la elimu na uhusiano wake katika mila huamsha mashaka yasiyo ya kawaida kwa baadhi ya watu nchini Tanzania, hata wakatenda mambo kama vile wao ni viumbe wapya duniani. Wanakuwa na wasiwasi kwamba elimu itaathiri maisha na desturi za familia zao na kipato. Kinyume na hao, wazazi waliopevuka kifikra husema kuwa mbingu ndiyo kikomo cha shauku za watoto kufikia upeo wa elimu wanayotaka. 

Wanafunzi wachache waripoti shule za sekondari, Tanzania

This browser does not support the audio element.

Hapo najiuliza, kwa nini kila mwaka serikali hupoteza muda na rasilimali kuwatafuta kila upande wanafunzi wasioripoti shuleni na nafasi zao hubaki wazi bila sababu ya maana. Ni haki kwa kila mtoto kupata elimu na ni wajibu wa wazazi kuwafuatilia wakiwahimiza kusoma.

Lakini kama ilivyo ada ya kila mwaka, wakuu wa shule wameanza kutoa taarifa za kushangaza kuhusu idadi ya wanafunzi watoro ambao bado hawajaripoti shuleni walikopangiwa. Madarasa yalijaa nusu hadi mwisho wa juma la pili la masomo.  Viongozi wa serikali za mitaa wakiandama na walimu wako mbioni kuwasaka wanafunzi hao.

Rais Samia Suluhu Hassan ametanka wazi wazi kwamba serikali haitamuacha mtu yeyote anayeingilia kuharibu elimu ya watoto wa Tanzania, hasa wasichana, ambao wanahitaji mazingira safi ya kuwafikisha kwenye malengo yao katika maisha.

Viongozi wa mitaa na Wizara ya Elimu walitakiwa kuandaa vifaa muhimu vya kufundishia na kusoma shuleni, kama vile vitabu na vifaa vya kuandikia, kabla ya mwaka wa masomo kuanza. Afisa yeyote atakayekutwa alizembea katika hili, ni wazi kabisa atapata wakati mgumu.

Wanafunzi katika shule ya sekondari ya Ingwe huko Mara Tanzania mwaka 2012Picha: DW/J. Hahn

Kurundikana kwa wanafunzi katika madarasa limekuwa tatizo sugu nchini, pamoja na uhaba wa fenicha na nyumba za walimu, na ukosefu wa maliwato, hasa maeneo ya vijijini. Mlundikano wa wanafunzi ni jambo ambalo pia limechangiwa na kuongezeka haraka kwa idadi ya watu na uhamiaji kutoka vijiji vya mbali kwenda makazi mapya kando ya barabara na maeneo yanayotarajiwa kuwa na shughuli mpya za kiuchumi, hasa uchimbaji wa madini.

Wingi wa wanafunzi shuleni mwaka huu ni mafanikio ya serikali ambayo imetumia fedha nyingi kujenga shule mpya na kukarabati majengo ya shule yaliyokuwa katika hali mbaya.

Inaripotiwa mara nyingi kuwa wasichana na wavulana wa Tanzania hurubuniwa kuacha masomo, ama kwa kushirikiana na wazazi au jamaa zao, mahali pengine na watu wenye tamaa ya pesa za mteremko.

Wasichana wadogo huozwa bila kupata ushauri wowote kuhusu ndoa, wavulana nao wanapelekwa kufanya vibarua sehemu za mbali na nyumbani kwao katika mashamba, machimbo ya madini na shughuli nyingine zisizo rasmi. Wote hupotoshwa na watu wenye tamaa binafsi kutajirika kirahisi. Baadhi ya wasichana wameripotiwa kupata ujauzito wakati wakisubiri kuingia kidato cha kwanza mwaka huu.

Happy Sanga shujaa wa ukombozi wa wanafunzi

05:24

This browser does not support the video element.

Kwa kuwa taifa hili limezingatia elimu kwa miaka mingi, ni jambo la kipuuzi kuona bado baadhi ya watu mbumbumbu wakiwazuia watoto wadogo kwenda shule. Tanzania tayari inazo taasisi za elimu ya hali ya juu na zenye hadhi ya kimataifa, mbali ya kuwa na wataalam ambao wanasifika katika fani mbalimbali zikiwa pamoja na utabibu, uchumi na sayansi ya mambo ya angani. Katika hali ya sasa taifa letu haliwezi kutamani lolote chini ya hapo.

Hata hivyo bado tuna watu wasioami elimu ya kisasa na watabaki kudorora nyuma katika maendeleo ya binadamu. Mathalan, watu hao wanapopata maradhi, huenda hospitali kupata matibabu. Wanatibiwa na waganga wa umri ule ule au wadogo zaidi wakilinganishwa na watoto wao ambao waliwanyima fursa ya kupata elimu.

"Nataka watoto wangu wafanye vizuri zaidi katika elimu kuliko mimi nilipohitimu elimu ya sekondari,” alisema mstaafu mmoja, akiwahimiza binti wawili ambao wanatarajia kufanya mitihani ya kumaliza masomo ya sekondari mwaka huu. "Tunawataka wafanye vizuri katika masomo. "Wakitiwa moyo na mashujaa wao, na sisi wazazi hatuna budi kufuatilia safari yao ya elimu kwa kuwashauri kutokana na uzoefu wetu wenyewe.”

Serikali imetimiza kazi yake kuweka mazingira wezeshi katika kila sekta ili wananchi washiriki kuleta maendeleo na ufanisi. Katika jitihada hizo imetanguliza elimu, ikitegemea ubia na washiriki wenye nia ya kuchangia ukuaji wa elimu ya vijana.

Wanafunzi wakinyoosha mkono kujibu swali darasani huko Lindi TanzaniaPicha: picture-alliance/robertharding

Kama taifa linaloendea, Watanzania wanahitaji kuwa na maono ya pamoja katika kutafuta majibu ya masuala yahusuyo umasikini, kama vile stadi muhimu, mawasiliano, ukosefu wa usalama wa chakula na ustawi wa jamii.

Wakiwa na dhamira ya kufuta ujinga, viongozi wa serikali ya uhuru nchini Tanzania walianzisha programu ya elimu ya watu wazima ambayo iliwezesha maelfu ya wasiojua alfabeti kujiunga na jamii ya wasomi.

Ili kuendeleza muamko huo, ingefaa ikiwa watungasera na viongozi wa jamii watafufua mpango wa elimu ya watu wazima ambao utawezesha idadi inayoongozeka ya watu wasiojua matumizi madogo madogo ya sayansi na teknolojia kwenda pamoja na ulimwengu wa kisasa.

Kuwabakiza watu hao nyuma kutamaanisha kero kubwa baadaye jinsi serikali na watoa huduma kwa umma wanavyoboresha shughuli zao haraka kwa kutumia teknohama. Wanatengeneza mifumo ya kisasa kutoa huduma katika benki, usafiri na uuzaji bidhaa aWajawazito kurejea shuleni Tanzaniambayo haiwezi kuchepushwa wala kuzimwa ili kuwasubiri mbumbumbu.

Kuingilia mifumo hii kutamaanisha tu ukosefu wa mapato na huduma. Tunahitaji kuboresha sera ya elimu na kuwaokoa wasiojua teknojia za mawasiliano wasibaki nyuma wakati tukijitahidi kwenda sambamba na wabia wetu walio mbele zaidi katika dunia hii.

Kwa hiyo, mawasiliano yasiwe changamoto ya kudumu katika kukuza biashara za Tanzania, ukuzaji wa viwanda na mageuzi ya kidigitali. Lazima tufanye kazi pamoja kutimiza majibu yanayoendana na matakwa ya watoto na vijana wa taifa hili.