1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barua kutoka Dar: Ndoto ya taifa la viwanda

Sylvia Mwehozi
3 Machi 2018

Wasomi wa Tanzania wamejitolea miaka mingi ya kazi ili kugundua mambo ambayo hayajulikani katika fani mbambali. Wanajitahidi kuongeza ujuzi wa kisayansi katika sekta mbalimbali.

Tansania Dar Es Salaam Kigamboni Brücke Hängebrücke
Picha: Imago/Xinhua

Na Anaclet Rwegayura

Wasomi wa Tanzania wamejitolea miaka mingi ya kazi ili kugundua mambo ambayo hayajulikani katika fani mbambali. Wanajitahidi kuongeza ujuzi wa kisayansi katika sekta mbalimbali zikiwa pamoja na kilimo, uhandisi ujenzi, dawa, uvumbuzi wa vitu, ujasiriamali na mambo mengine mengi.

Pamoja na kutumia muda wao wote na nguvu kuchunguza yasiyojulikana , ni kama vile wanakwaruza uso wa dunia bila kupiga hatua mbele, angalau, kupata ufumbuzi wa matatizo yanayolikabili taifa kuhusu maendeleo. Hii inamaanisha bado wanahitaji msaada zaidi kutoka kwa umma na watu biinafsi ili taifa lisonge mbele katika mchakato huu wa pole pole kuanzisha viwanda.

Fedha nyingi zimeishamwagwa na Serikali pamoja na wahisani wa maendeleo katika shughuli za utafiti, lakini, ama yamekuwepo matokeo kidogo ya kusifia au hakuna kitu cha kuonesha.

Bandari ya Dar es salaam ambayo inategemewa sana nchi jiraniPicha: Getty Images/Keystone

Ingawa baadhi yao wanaweza kujisikia wamekosa walichokusudia, lengo la kawaida la watafiti ni kuwezesha  watu kuishi maisha bora katika mazingira ya kisasa.

Umma umesikia mengi kuhusu tafiti zilizofanywa na vituo vya kitaaluma vya Tanzania kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na taasisi nyingine za elimu ya juu nchini.

Lakini ni kwa mafanikio yapi makuu  ambayo watafiti  wa Tanzania wamedhihirisha kuleta matokeo katika uchumi au katika ustawi wa watu na utamaduni wao?

Kutambua haja ya kuwa na uchumi unaozingatia viwanda kumesababisha mijadala mingi kuhusu aina ya viwanda vinavyoweza kuleta utajiri zaidi na ajira nchini. Bado Watanzania wengi wanatatanishwa na dhana inayopigiwa debe sana  ya "uchumi wa viwanda”.

Kwa upande mmoja, umma unahitaji kuelimishwa kuhusu mfumo wa uchumi unaotegemea viwanda na dhima yake katika maendeleo. Je, mfumo huo utawezesha kuongeza thamani kwa kila bidhaa au kila huduma itakayotolewa? Upande mwingine, Watanzania wanatazamia serikali yao kuweka sera ya mafanikio ya viwanda, ikilenga mauzo ya nje ya nchi na pia soko la ndani.

Kwao, haipaswi kusubiri zaidi wakikodolea macho  nchi ambazo tayari zimefanikiwa katika viwanda. Tanzania ina rasilimali nyingi za asili na mali ghafi kwa ajili ya viwanda.

Sasa ni juu ya watunga sera, watafiti na wawekezaji watarajiwa kuweka juhudi zao na vichwa vyao pamoja ili kutumia vizuri rasilimali hizi katika viwanda kwa manufaa ya taifa. Ni jambo wazi kwamba Watanzania hawawezi kuondokana na umasikini wao bila kuwa na viwanda na biashara katika bidhaa za viwandani pamoja na kiwango cha juu cha ubora wa huduma.

Ni muhimu kwa wawekezaji na serikali kukubaliana juu ya mikakati ya makusudi  kuharakisha maendeleo ya viwanda, kwa kuzingatia upungufu wa sasa wa ujasiriamali wa sekta ya umma na binafsi.

Rais wa Tanzania John Magufuli na mwenzake wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed SheinPicha: DW/Y. Talib

Licha ya shauku ya umma kushuhudia wito usioisha wa kisiasa kuhusu uwekezaji katika viwanda ukitimia na kuwa na umbo la biashara, Watanzania hapana budi watambue kwamba tofauti kati yao na mataifa mengine  haitegemei upatikanaji wa rasilimali za asili au ukubwa wa nchi, bali zaidi ni ya mtazamo wa kufanya kazi na kuwa na mazao, kuweka akiba na kuwekeza -- yote yakikuzwa kwa miaka ya elimu na utamaduni.

Uwekezaji wowote ambao unalenga maendeleo ya viwanda usichezewe kama kamari. Yote yapangwe kwa uadilifu na kuchukua hatua. Sekta zote zitahitaji ufuatiliaji mkali na uwezo wa juu zaidi wa utawala ili kuleta matokeo yanayotarajiwa.

Itakuwa vyema kwa Tanzania kutambua au kuanzisha asasi za maendeleo za kisekta kama sehemu muhimu ya kuendeleza sera yake ya viwanda. Taasisi hizo zimekuwa na jukumu muhimu katika kusaidia viwanda maalum katika nchi zilizoanzisha mifumo ya viwanda karibuni kama vile Korea ya Kusini na Taiwan, kwa ajili ya kukuza mauzo ya nje, kuendeleza  ujuzi, utafiti na maendeleo, na uratibu ulioimarika.

Jirani na hapa, Ethiopia imetumia mazoezi haya kwa kuanzisha Taasisi ya Maendeleo ya Sekta ya Ngozi mwaka 2010 na asasi nyingine za nguo, vyakula na vinywaji, dawa, na kemikali, nk.

Ingawa bado ni changa ikilinganishwa na ‘Chui wa Asia', Ethiopia imeandika sura mpya ya maendeleo yake kwa kuanzisha mfumo wa maendeleo ya viwanda hivi karibuni. Tanzania inaweza kupata somo kutokana na uzoefu wa Ethiopia, ambayo mara kwa mara husisitiza kuwa nchi za Afrika zinapaswa zenyewe kuongoza maendeleo yao.

Inasemekana kuwa kujifunza kwa vitendo ndiyo njia kuu ya kumudu uzalishaji katika nchi zilizochelewa kujenga viwanda. Lengo na jukumu la sera ya viwanda Tanzania inapaswa iwe kuongeza kasi ya kujifunza wakati nchi  ikichonga mwelekeo wake.

Baada ya mwaka 2025, Watanzania wanatarajia kuona mazingira mapya ya viwanda vinavyovuma kwa kishindo kila mji, bidhaa za ndani zikijaa madukani na nyumbani. Hapo vyombo vya habari vitatangaza kwa ujasiri ujumbe wa mali 'Imetengenezwa Tanzania'. Hii ni kama hadithi ya ndoto ya kusadikika!

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW