1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen kuweka historia isiyofutika kirahisi?

21 Mei 2024

Bayer Leverkusen ya Ujerumani yabakiza mechi mbili tu kuandika historia ambayo haijashuhudiwa katika kandanda.

Bundesliga | Kocha wa Leverkusens Xabi Alonso
Kocha wa Bayer Leverkusen Xabi Alonso akiwa amenyanyua kombe la Bundesliga la kwanya kwa klabu hiyoPicha: Michael Probst/AP Photo/picture alliance

Mabingwa hao wapya wa Ujerumani wanakabiliwa na mechi za fainali za michuano miwili katika siku hizi nne kuanzia leo Jumatano wanapokutana na Atalanta kuhitimisha michuano za Ligi ya Ulaya ama Europa League na kuhitimisha kabisa ile ndoto ya kumaliza msimu wa ligi kuu ya ndani ya Bundesliga na hata michuano ya mabara bila ya kufungwa.

Leverkusen siku ya Jumamosi itakutana na timu ya Kaiserslautern katika fainali za kombe la Shirikisho la Ujerumani  DFB- Pokal na kwa hakika inapewa nafasi kubwa ya kushinda, kwa sababu sio tu itapambana na timu iliyomaliza msimu ikiwa nafasi ya 13 katika ligi ya daraja la pili, bali pia iliponea chupuchupu kuingia kwenye kundi la mechi za kufuzu ili kuepuka kushuka daraja.

Na sasa kizingiti kikubwa kwa kocha wa Leverkusen Xabi Alonso ni mchezo wa 52 kati ya 53 utakaopigwa huko Dublin dhidi za Atalanta na ambao utahitimisha msimu wao wa ndani na nje wakiwa ngangari.

Na pengine wataudhibiti mchezo huo kwa sababu Ligi ya Ulaya imekuwa kama mchezo wa kuigiza hivi kwa Leverkusen.

Wachezaji wa Leverkusen wakiongozwa na Jonathan Tah baada ya kukabidhiwa kombe la ubingwa wa Bundesliga, 2024Picha: Ina Fassbender/AFP/Getty Images

Lakini kumekuwepo na timu nyingine zilizofanya vizuri katika michuano ya Ulaya kwa kushinda ligi ya Mabingwa Ulaya na taji la ligi ya ndani, tofauti na Leverkusen inayocheza mashindano ya daraja la pili ya Ulaya, Europa League.

Lakini isingekuwa ajabu kuona mafanikio kwa klabu tajiri kama Manchester United mnamo mwaka 1999, Inter Milan mwaka 2010, Barcelona kwa mwaka 2011 na Manchester City kwa mwaka uliopita. Kila klabu ilianza msimu ikiwa na wachezaji nyota wa kutisha huku zikiongozwa na makocha kama Sir Alex Ferguson, Jose Mourinho, Pep Guardiola ambaye tayari ameshinda makombe kadhaa ya ligi ya Premier na Ulaya.

Msimu huu mzima na wa kwanza wa Alonso kwa hakika ulikuwa ni wa kiwango cha juu. Kikosi chake kilikuwa katika hatihati ya kushuka daraja msimu uliopita. Na hakukua na mchezaji nyota yoyote aliyesaini wakati wa mapumziko kukipiga na Leverkusen.

Kocha huyo mwenye miaka 42 alisema wiki iliyopita kwamba hatua hii ni muhimu sana kwake. Akaongeza kuwa kombe langu la kwanza kama kocha Bundesliga. Ilikuwa ni kitu cha muhimu sana. Lakini kombe la Ulaya litakuwa ni bora hata zaidi, na kusema wana uhakika watashinda.

Alonso alishinda mara mbili ubingwa wa Champions wakati huo akiwa kiungo wa Liverpool na Real Madrid ambayo itakwaana na Borussia Dortmund kwenye fainali za mwaka huu za Champions, Juni Mosi katika uwanja wa Wembley huko England.

Real Madrid ya Uhispania ni moja ya timu zenye mafanikio makubwa kisoka barani Ulaya. Picha: Juan Medina/REUTERS

Wakati mwaka 2002, Leverkusen ilishindwa kutamba katika fainali ya Ligi ya Mabingwa, dhidi ya Madrid, Atalanta iliikaribia nusu fainali ya mwaka 2020, ingawa kwa ujumla timu hizo hazikutajwa kama miongoni mwa timu zenye mafanikio katika soka la Ulaya.

Viwanja vyao vya kawaida tu vilivyopo mjini Leverkusen na Bergamo kwa pamoja vina uwezo wa kuchukua mashabiki 51,000 ambao wanaweza kutosha kwenye uwanja wa Dublin ambao ambako watakutana na Atalanta.

Vilabu hivi vya Leverkusen na Atalanta hata sio miongoni mwa vilabu 50 vya Ulaya vyenye mapato makubwa hii ikiwa ni kulingana na utafiti wa Shirikisho la Soka barani Ulaya, UEFA.

Vilabu hivi viwili vinategemea mikataba ya uhamisho wa wachezaji na kampuni kubwa ya dawa Bayer na Boston ambaye ni mmiliki mwenza wa Celtics, Steve Pagliuca.

Atalanta ambayo imekuwa ikifundishwa na kocha Gian Piero Gasperini tangu mwaka 2016 tayari imejihakikishia kushiriki michuano ya Champions msimu ujao.

Lakini kile ilichokifanya Leverkusen sio cha kawaida, na zimebakia siku chache tu kuandikwa historia ambayo si rahisi kuvunjwa.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW