Bayer yainunua Monsanto
7 Juni 2018Makampuni hayo sasa yameunda kampuni kubwa kabisa la madawa ya kilimo likiwa na dhamira kubwa ya kuilisha dunia lakini wakati huo huo ikishambuliwa na wanaharakati wanaotetea mazingira.
"Kulisha idadi ya watu inayoongezeka duniani ni lengo lake la muda mrefu, na tunataka kuchangia katika utatuzi wa suala hilo," mtendaji mkuu wa kampuni ya Bayer Werner Baumann aliliambia gazeti la masuala ya biashara la Handelsblatt katika mahojiano siku ya Jumanne. Watendaji wanatabiri mambo makubwa katika makadirio kwamba kiasi ya watu bilioni 10 watakuwa wanaishi katika dunia hii ifikapo mwaka 2050, ikiwa na maana ya kwamba chakula kingi zaidi kinalazimika kulimwa katika eneo lile lile la ardhi inayoweza kulimwa.
Wanasema hilo linawezekana kufanikishwa kwa njia bora zaidi kwa kutumia teknolojia zinazopuuzwa na mashirika ya ulinzi wa mazingira pamoja na wanasiasa, ikiwa ni pamoja na mbegu zilizobadilishwa vinasaba ambazo zimetayarishwa kwa kupambana na madawa makali ya kuuwa wadudu.
Mimea iliyobadilishwa vinasaba pamoja na vifaa vya digitali kuwasaidia wakulima waweze kujiweka katika hali ya kupambana na hali ya hewa na kuangalia afya ya mashamba yao kunaweza pia kusaidia kuongeza mazao ambayo yanatishiwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Malengo endelevu
"Tutawasaidia wateja wetu kulima mazao mengi zaidi kwa gharama nafuu," Baumann aliwaambia waandishi habari siku ya Jumatatu, wakati huo huo akiahidi kwamba " tutaweka msukumo huo huo katika kufanikisha malengo yetu endelevu kama tunavyofanya katika malengo yetu ya kifedha."
"Suala muhimu litakuwa iwapo Bayer ni imara vya kutosha kujitenganisha," gazeti la Handelsblatt limetabiri.
"Kwa upande mmoja ni wa biashara ambapo ni muhimu kupata fedha nyingi za kutosha kwa ulinzi wa mimea kupitia madawa na mbegu kama wanavyotaka wawekezaji. Kwa upande mwingine , Bayer inahitaji kupata kuaminika na umma ambao unaendelea kuwa shaka shaka juu ya kilimo kinachoongozwa na viwanda.
Kufuatia kuungana kwa Dow na DuPont mwaka 2017 na ChemChina kununua kampuni la Uswisi la Syngenta , kujapamoja kwa Bayer na Monsanto ni muungano mkubwa kabisa katika wimbi la makampuni makubwa kuungana katika viwanda vya kemikali ambayo yameunda muungano mkubwa kabisa katika bara la Ulaya, Marekani na Asia.
Tangu ilipozinduliwa mwaka 2016, ndoa hii ya Bayer na Monsanto itaunda kundi kubwa kabisa la makampuni likiwa na wafanyakazi 115,000 na mapato ya kila mwaka ya euro bilioni 45.
Maafisa wanaoangalia ushindani waliilazimisha Bayer kuuza sehemu ya biashara yake ya hivi sasa ya mbegu na madawa ya kilimo, ambayo yalikuwa yanaiingizia kampuni hiyo kiasi cha euro bilioni 2.2 kwa mwaka , kwa kampuni washindani wake la BASF kabla ya kuruhusu makubaliano hayo.
Bayer ina nia ya kupunguza mbinyo kutoka kwa walinzi wa mazingira na wanasiasa kama ilivyo kwa wawekezaji pia. Upinzani duniani kote dhidi ya kilimo kinachoendeshwa na viwanda na hususan Monsanto umesababisha watendaji kutangaza wiki hii kwamba jina hilo linaachwa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Iddi Ssessanga