1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern na Barcelona zatamba Ulaya

25 Novemba 2015

Bayern Munich ilijikatia tikiti ya duru ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuicharaza Olympiacos ya Ugiriki mabao manne kwa sifrui. Waliutawala mchezo licha ya kubakia wachezaji kumi katika kipindi cha pili

Fußball UEFA Champions League FC Bayern München - Olympiakos Piräus
Picha: Getty Images/Bongarts/M. Hangst

Wakati Bayern wakimaliza wa kwanza katika Kundi F, Arsenal iliyaweka hai matumaini yake kwa kuinyuka Dinamo Zagreb mabao matatu kwa sifuri uwanjani Emirates, maana kuwa wanaweza kufuzu ikiwa watashinda dhidi ya Olympiakos mwezi ujao kwa angalau kufunga mabao mawili kwa sifuri au zaidi ya hapo.

Bayer Leverkusen ilitoka sare ya moja moja ugenini na BATE Borisov. Barcelona tayari imefuzu katika 16 za mwisho baada ya kuichabanga Roma magoli sita kwa moja jana, kumaanisha moja kati ya Leverkusen, katika nafasi ya pili na BATE katika nafasi ya tatu ya Kundi E ina fursa ya kufuzu pia. Lakini Leverkusen ina kibarua kigumu katika mchuano wa mwisho dhidi ya Barcelona wakati BATE ikialikwa na Roma.

Leverkusen ina kibarua katika mchuano wa mwisho dhidi ya BarcaPicha: Getty Images/AFP/M. Malinovsky

Mambo yanaonekana mazuri kwa Cheslea ambao walipata mabao manne kwa sifuri dhidi ya Maccabi Telaviv nchini Israel. Katika mchuano mwingine wa Kundi G, Dynamo Kiev ilishinda mbili sifuri dhidi ya Porto. Ni pointi mbili pekee zinazotenganisha Chelsea, Porto na Dynamo Kiev lakini vijana wa Jose Mourinho watahitaji tu sare dhidi ya Porto ili kufuzu. Zenit St Petersburg, ambao tayari walikuwa wamefuzu kwa hatua ya mchujo, waliwazaba Valencia mbili sifuri katika Kundi H. Gent iliiruka Valencia hadi nafasi ya pili baada ya ushindi wa mbili moja ugenini dhidi ya Lyon ambao uliibandua timu hiyo ya Ufaransa nje ya dimba hilo.

Hii leo Wolfsburg itacheza ugenini dhidi ya CSKA Moscow wakati Borussia Moenchengladbach ikiwa nyumbani dhidi ya Sevilla.

Real Madrid na Manchester City, ambao wanacheza leo tayari walijikatia tikiti ya 16 za mwisho. Malmo itachuana na Paris St Germain huku Shakhtar Donetsk ikiangushana Real Madrid

Manchester United itaikaribisha PSV Eindhoven. Astana watapiga dhidi ya Benfica, Atletico Madrid watawaalika Galatasaray wakati Juventus ikifunga kazi dhidi ya Manchester City

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo