Ni mchuano wa kwanza wa Der Klassiker msimu huu
3 Oktoba 2015Bayern Munich wamezishinda mechi zote zaba za Bundesliga, hiyo ikimaanisha kwamba tayari wana pointi zao zote 21 kibindoni. Borussia Dortmund kwa upande mwingine wametetereka kidogo na kutoka sare mechi zao mbili za mwisho, baada ya kushinda tano za awali. Kwa maana hiyo, klabu hiyo inazo pointi 17, ikizidiwa pointi nne na Bayern Munich.
Hapa Ujerumani mechi kati ya timu hizo mbili inajulikana kama Der Klassiker, na ichezwapo, basi kwa mashabiki wa soka, shughuli nyingine husimama. Siyo tu kwamba timu hizi zinakaribiana kwa pointi zilizozikusanya msimu huu, bali pia idadi ya magoli yaliyoingizwa na washambuliaji wao haijapishana sana. Robert Lewandowski wa Bayern Munich anaongoza kwa kupachika mabao 10 yakiwemo 5 aliyoyaingiza katika muda wa dakika 9 dhidi ya Wolfsburg wiki chache zilizopita, na anayepumua kisogoni mwake ni Pierre-Emerick Aubameyang wa Dortmund, ambaye amekwizamisha kimiani magoli tisa.
Kocha wa Borussia Dortmund Thomas Tuchel amewapumzisha wachezaji wake 5 katika mechi ya Europa League dhidi ya PAOK Salonika, ili kuhakikisha kikosi chake kiko 'Fit' asilimia mia moja kuweza kuikabili Bayern Munich. Si kazi rahisi, lakini bila shaka anaweza kuwa na matumaini, kwa kuzingatia kwamba msimu huu hajapoteza mechi yoyote inayohitaji pointi. Mechi hiyo kati ya Bayern Munich na Borussia Dortmund itaanza saa kumi na moja na nusu muda wa Afrika Mashariki, kesho Jumapili.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre/ape
Mhariri:Mohammed Abdul-rahman