1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern kukwaruzana tena na Real Madrid

11 Aprili 2014

Droo ya mechi za nusu fainali ya Champions League, ilizileta pamoja timu mbili maarufu Ulaya ambazo zimekuwa na utani wa tangu jadi na kuyaweka hai matumaini ya kuwepo fainali ya watani wa mjini wa Madrid.

Schweiz Fußball UEFA Champions League 2014 in Nyon Luis Figo
Picha: Getty Images

Mabingwa watetezi wa kombe hilo Bayern Munich watakutana na washindi mara tisa Real Madrid. Bayern wanalenga kuwa timu ya kwanza kuhifadhi taji hilo la Ulaya ambalo limedumu misimu 22.

Vijana hao wa Pep ambao tayari ni mabingwa wa Ujerumani walikutana na Real katika nusu fainali mwaka wa 2011/2012. Walishinda mechi hiyo kwa mikwaju ya penalty mjini Madrid kabla ya kushindwa na Cheslea katika fainali. Miamba hao wa soka Ulaya wamekutana mara tano katika nusu fainali, huku Bayern ikishinda mara nne.

Wakati Bayern wakilenga kushinda taji la Ulaya kwa mara ya sita, wanajaribu kufikia fainali yao ya nne katika miaka mitano, nao Atletico wanalenga kufikia fainali kwa mara ya kwanza.

Viongozi hao wa Laliga wamezawadiwa mchuano wa nusu fainali na Chelsea baada ya kuwabandua nje Barcelona. Chelsea na Atletico zilikutana mwaka wa 2012 katika mcnhuano wa Super Cup ambapo Atleti walishinda magoli manne kwa moja.

Atletico Madrid watalenga kuendeleza ndoto yao nzuri msimu huu kwa kuwazima ChelseaPicha: Getty Images

Mourinho anajaribu kuwa kushinda taji hilo kwa mara ya tatu na timu tatu tofauti baada ya Porto na Inter Milan.

Kabla ya droo, Shirikisho la soka Ulaya – UEFA liliionya Chelsea kuwa ni lazima wasiizuie Atletico kumtumia mlinda lango wao Thibaut Courtois ambaye anaichezea Atleti kwa mkopo kutoka Chelsea.

UEFA imesema kipengele chochote katika mkataba wa mkopo wa Courtois kinachomzuia kushiriki mchezo huo ni kinyume cha sheria za mchezo. Courtois amekuwa mchezaji muhimu kazika msimu wa kufana wa Atletico. Mechi za mkondo wa kwanza zitachezwa mnamo Aprili 22 na 23 huku zile za marudiano zikichezwa Aprili 29 na 30.

Kwingineko, Juventus wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kucheza fainali ya Europa League katika uwanja wao wa nyumbani baada ya kupangwa dhidi ya viongozi wa ligi ya Ureno Benfica katika nusu fainali. Sevilla watapambana na Valencia katika mchuano mwingine. Mechi za mkondo wa kwanza zitachezwa Aprili 24 huku za maridioano zikichezwa Mei mosi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu