Bayern kuponyoka na taji la Bundesliga
24 Machi 2014Bayern wana uongozi wa pengo la points 23 na hawawezi kufikiwa na Borussia Dortmund au Schalke kama watapata ushindi wao wa 25 katika mechi ya 27 msimu huu katika mechi yao ya kesho Jumanne 25.03.2014 dhidi ya Hertha Berlin katika uwanja wa Olympic stadion, mjini Berlin.
Kummwagia kocha glasi kubwa za bia za jimbo la Bavaria ndiyo njia ya kitamaduni kwa wachezaji wa Munich kusheherekea taji lao, na Guardiola atakuwa mwathiriwa mpya. Mwishoni mwa wiki Bayern waliwashinda Mainz magoli mawili kwa sifuri na hawangeweza kutawazwa washindi kwa sababu mahasimu wao Schalke na Dortmund pia walishinda.
Katika mechi nyingine ya kukata na shoka, mabingwa wa mwaka wa 2011 na 2012 Dortmund ambao wana points 51 wanashuka dimbani dhidi ya mahasimu wao Schalke ambao wana points 50, ijapokuwa timu zote mbili zina matatizo ya majeruhi. Schalke wako mbele ya Bayer Leverkusen ambao wana points 44 baada ya kuchabangwa na Hoffenheim hapo jana magoli matatu kwa mawili, na ni lazima wang'ang'anie nafasi ya Champions League na Borussia Moenchengladbach ambao wako nyuma yao na tofauti ya points tatu pekee, nao Wolfsburg na Mainz wakiwafuata na tofauti ya points nne. Mshambuliaji wa Schalke Klaas-Jan Huntelaar anasema wamejiamini vilivyo kwa mchuano huo wa kesho dhidi ya BVB
Vijana wa Sami Hyppia, Leverkusen wako chini ya shinikizo baada ya kushinda mechi mbili pekee kati ya tisa tangu kurejea kutoka mapumziko ya kipindi cha baridi, na lazima wafanye vyema dhidi ya Augsburg siku ya Jumatano.
Kuepuka shoka la kushushwa daraja
Lakini sarakasi yenyewe iko katika upande wa chini wa msimamo wa ligi, ambako nusu ya ligi inapambana kubaki hai. Hoffenheim inaonekana iko salama ikiwa na points 32 pamoja na Hanover, Frankfurt na Werder Bremen, ambao wana points 29 kila mmoja. Points nne chini, Freiburg wako na 25, VfB Stuttgart wana 24, SV Hamburg wana 23 na katika eneo la kushushwa daraja. Nuremberg pia 23 na Eintracht Braunschweig 18 katika nafasi mbili za mwisho, na hiyo ina maana wanadondoka moja kwa moja.
Sasa siku ya Jumatano, Hamburg watakuana na Freiburg, nao Nuremberg wapambane na mabingwa wa 2007 Stuttgart huku Hamburg ikijaribu kwa udi na uvumba kuepuka kushushwa daraja kwa mara ya kwanza tangu Bundesliga ilipoanzinshwa mwaka wa 1963.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu