1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern mabingwa tena Bundesliga

Sekione Kitojo
9 Aprili 2018

Bayern Munich  yanyakua rasmi  ubingwa  wake  wa  sita  mfululizo katika  Bundesliga ,  Borussia  Dortmund yajisahihisha  na kuimarisha  nafasi  yake  ya  kucheza  Ulaya.

Fußball Bundesliga FC Augsburg - FC Bayern
Picha: Imago/kolbert-press/C. Kolbert

Bayern Munich  imetia  kibindoni taji  lake  la  28 la  Bundesliga  wiki hii  baada  ya  kutawazwa  tena  kwa  mara  ya  sita  mfululizo  kuwa mabingwa  siku  ya  Jumamosi  baada  ya  kuikandika  Augsburg kwa  mabao  4-1.  Bayern  imedhihirisha  kwamba  wao  ni  washindi wasioshindia  katika  Bundesliga.

Wachezaji wa Bayern Frank Rebery (katikati) na Rafinha wakishangilia ubingwa wa timu yao ya Bayern Picha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Sherehe  za  Bayern  hata  hivyo zilionekana  kuwa  katika  hatari  ama  kucheleweshwa  wakati  mlinzi wao Niklas Sulle  alipouweka  mpira  katika  wavu  wake. Hata  hivyo Corentin Tolisso na  James Rodriguez  walipachika  mabao  ya haraka  kwa  mabingwa  hao  kabla  ya  mapumziko  na  kisha  Arjen Roben  na  Sandro Wagner  walimalizia  katika  kipindi  cha  pili.

Bayern  ambayo  ina  pointi 72 kutoka  michezo  29  ya  bundesliga msimu  huu, imefungua  mwanya  wa  pointi 20  kutoka  timu  iliyoko nafasi  ya  pili  Schalke 04, ambayo  ilipokea  kipigo  bila  kutarajiwa cha  mabao 3-2 dhidi  ya  timu  iliyoko  mkiano  ya  Hamburg SV.

Ilikuwa  ni  mafanikio  makubwa  ya  binafsi  kwa  kocha  mwenye umri  wa  miaka 72  wa  Bayern  Jupp Heynckes , ambaye  alitoka katika  kustaafu  mwezi Oktoba  na  kuchukua  nafasi  ya  Carlo Ancelotti  akirejea  mara  ya  nne  katika  klabu  ya  Bayern wakati timu  hiyo ikiwa  nyuma  kwa  pointi  tano  dhidi  ya  Borussia Dortmund.

Kocha Jupp Heynckes wa bayern MunichPicha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

„Nilikuwa  na  imani kwamba, tunaweza  kubadilisha  mambo. Ilikuwa katika  wakati  huu Borussia  Dortmund  ikiongoza  kwa  pointi 5 na ilicheza vizuri  sana. Na  ndio  sababu watu hawakudhani  kwamba , hivi sasa tungekuwa  mabingwa wa  Ujerumani. Tumepiga  hatua  kubwa  sana. Hata mimi  binafsi  sikufikiria  hivyo, badala  yake  kwangu  ilikuwa  wazi , kwamba tujiimarishe tu pale tulipo."

Licha ya kwamba sherehe  za  ubingwa  hazikuwa  kama  miaka  yote, kutokana  na  majukumu  mengine  kama  ya  champions league  na kombe  la  shirikisho  nchini  Ujerumani DFB, lakini wachezaji  waliruka ruka uwanjani  mjini  Augsburg  kuashiria  kwamba  bado  wana  uchu wa kunyakua  mataji  mengi  zaidi. Arjen Robben  aliyefunga  bao  alikuwa  na haya  ya  kusema.

„Ubingwa  ni  ubingwa tu. Tumeshuhudia  baada  ya  kubadilisha  kocha tulikuwa  pointi 5  nyuma  ya  Borussia  Dortmund. Na  nasema  kila wakati, kila  mtu  anasema Bayern ina  kikosi kizuri sana, msimu  huu tumekwenda  mbali  zaidi, na hili linaeleza  kila  kitu. Lakini  kile  ambacho mtu  hapaswi  kusahau ni  kwamba  katika  Bundesliga  hupati matokeo kama  zawadi kwa  kuwa  tunafanyia  kazi. Wakati  ukiwa  huko vizuri kimchezo, huna umakini  huwezi pia kushinda  mchezo."

Arjen Robben (kushoto) wa Bayern Munich akijaribu kumtoka mlinzi wa Augsburg Martin HinterreggerPicha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Hamburg ambayo imekuwa  katika  historia  ya  miaka  55  ya   ligi  ya Ujerumani  Bundesliga , imesogea  juu  kidogo mwishoni  mwa  juma  hili kutoka  mkiano  kabisa  mwa  ligi na  kujipa  matumaini  madogo  ya kujinasua  kutoka  kushuka  daraja  wakati  ilipoishinda  Schalke 04  kwa mabao 3-2.

Timu  nyingine  iliyoko  mkiani  mwa  ligi FC Kolon  ilikuwa  na  matumaini ya  kutoroka  na  pointi zote  tatu katika  uwanja  wake  siku  ya  Jumamosi ilipotiana  kifuani  na  Mainz 05, ikiwa na  matumaini  ya  kujiongezea pointi  na  hatimaye  kujinasua  kutoka katika  hatari  ya  kushuka  daraja matumaini  hayo  yaliishia  ukingoni  baada  ya  kutoka  sare  ya  bao 1-1 katika  mchezo  mkali   nyumbani siku  ya  Jumamosi.

Borussia  Dortmund baada  ya  kubugizwa  mabao 6-0  na  mabingwa Bayern Munich  wiki  iliyopita, ilikuwa  bado  katika  fadhaa  ya  aibu  hiyo kubwa  iliyowakuta  msimu  huu. Na  baada  ya  kubabaika  katika  kipindi cha  kwanza  walijikongoja  na  kupata  ushindi usioridhisha  wa  mabao 3-0  dhidi  ya  timu  iliyopanda  daraja  msimu  huu  ya VFB Stuttgart.

Furaha ilirejea tena katika kikosi cha Dortmund baada ya kuikandika Stuttgart kwa mabao 3-0Picha: picture alliance/dpa/B. Thissen

Bado Dortmund haijathibitisha  hadhi  yake  ya  kuwa  nguvu  ya  pili  mbadala katika  Bundesliga  baada  ya  Bayern  na  msimu  huu  imesuasua  licha  ya kupata  ushindi  hapa  na  pale  bila  kuthibitisha  kwa  mchezo  safi  ambao umekonga  nyoyo za  mashabiki  wa  kandanda duniani.

Borussia  Moenchengladbach ilifanikiwa  kubadilisha  matokeo  kutoka kuwa  nyuma  kwa  bao 1-0 dhidi  ya  Hertha  Berlin  na  kupata  ushindi muhimu  wa  mabao 2-1 licha  ya  mashabiki  wa  timu  hiyo kulalamikia uchezaji  wa  timu  hiyo  na  jinsi  walivyopata  ushindi. Baada  ya  kuwa sare  kwa  bao 1-1, ghafla  mwamuzi Bibiana Steinhous aliombwa kuangalia  vidio kutoka  kwa  mwamuzi  wa  vidio na  kuurejesha  mpira katika eneo  la  adhabu  la  Hertha Berlin  na  kuwa  penati  ambayo Thorgan Harzad  aliuweka  wavuni  na  kuwa  bao  la  ushindi  kwa Moenchengladbach.

Ushindi  huo  hata  hivyo  haukuwafurahisha mashabiki  wake.  Kocha  Dieter Hecking  hata  hivyo  alisema amefurahishwa na ushindi  huo licha  ya  kucheza  chini  ya  kiwango.

Dieter Hecking wa Borussia MoenchengladbachPicha: SID

„Uwezo wetu katika  kipindi  cha  kwanza  haukufikia kiwango kinachotakiwa. Kila  mtu  uwanjani aliliona  hilo. Tulijiingiza  katika matatizo makubwa  katika ujenzi wa  mashambulizi  yetu. Ilionekana kwamba  hatukuwa  makini , licha  ya  kuwa  tulitaka  kucheza  kwa haraka zaidi. Hertha walitubana  sana. Tulikuwa  na matatizo, ambayo baada  ya  kufungwa bao, tungepaswa kujilinda  vizuri  zaidi, licha  ya kwamba  tuko  nyuma. Ilikuwa  wazi wakati wa  mapumziko, kwamba hatukuwa  na hamasa na  tuliwaambia, vijana jaribuni  kwa  njia  yoyote ile  kubadilisha  matokeo. Tuliweza  kweli kubadilisha matokeo. Ilikuwa hali ya kuonesha  dhamira , licha  ya  kuwa  hatukuonesha  mchezo wa hali ya juu."

Wachezaji wa RB Leipzig ambao watakuwapo uwanjani kupambana na LeverkusenPicha: picture-alliance/Fotostand/Ellerbrake

Leo Bundesliga  inakamilisha  mchezo wake  wa  29  ambapo RB Leipzig inaikaribisha  Bayer Leverkusen, timu ambazo ziko katika  nafasi  ya  5 na 6 zikipishana  kwa  pointi moja.

Wakati tunawapongeza  Bayern  Munich  kwa  ushindi  wa  taji  lao  la  sita la  Bundesliga  mfululizo , sasa mtazamo  unaelekea  katika  timu  kuwania kucheza  katika  Champions League  na  pia  kujinasua  kutoka  katika hatari  ya  kushuka  daraja.

 

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /rtre / dpae

Mhariri: Idd Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW